Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2015/16 imebaini ufisadi wa mabilioni ya fedha katika mradi wa chanjo ya Surua Rubella na ameshauri kufanyika uchunguzi wa kijinai na waliohusika warejeshe fedha hizo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hayo yalibainika wakati wa ukaguzi maalumu katika halmashauri za wilaya na ofisi za waganga wakuu wa mikoa.
Ukaguzi huo umebaini Sh20.9 bilioni zilipokelewa na Wizara ya Fedha kutoka Gavi Alliance na kiwango hicho chote kilipelekwa Wizara ya Afya kugharamia chanjo ya Surua Rubella.
Kati ya kiwango hicho, Sh19.09 bilioni zilitolewa kwa ajili ya chanjo; Sh18.3 bilioni zilitumika Tanzania Bara na Sh725 milioni zilipelekwa Zanzibar na Sh1 bilioni zilitumika kama gharama za uendeshaji.
Ripoti hiyo imeainisha kuwa hadi Desemba 31, 2014 kulikuwa na bakaa ya Sh838,423,408.
Fedha zilizopokelewa halmashauri
Ripoti hiyo inaainisha kuwa Sh17.3 bilioni zilitumwa katika mikoa na kuingizwa kwenye akaunti za Kifua Kikuu na Ukoma (TB & Leprosy) zinazosimamiwa na waganga wakuu wa mikoa husika isipokuwa Dar es Salaam.
Fedha hizo zilitolewa benki na kugawanywa zikiwa taslimu kwa maofisa wa mamlaka za Serikali za Mitaa ambao walikuwa wakihusika na chanjo.
Vilevile ripoti ilibaini kuwa Sh1 bilioni zililipwa kama masurufu kutoka Wizara ya Afya kwa ajili ya chanjo kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa Sh13.1 bilioni zilipokelewa na maofisa wa mamlaka za Serikali za Mitaa, wakati Sh1.07 bilioni zilizodaiwa kupelekwa katika mamlaka za Serikali za Mitaa hazikuthibitika kupokelewa.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa, maofisa wa Serikali za Mitaa walikana kufahamu ujio wa fedha hizo na nyaraka za mapokezi yake.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchunguzi huo ulibaini kuwa Sh2.1 bilioni zilibaki chini ya usimamizi wa maofisa wa Wizara ya Afya ambao walitumwa mikoani kwenda kusimamia chanjo.
“Hatukuweza kupata sababu za kubaki na kiwango hicho kikubwa cha fedha, wakati wao walikuwa ni waratibu tu wa chanjo,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ya ukaguzi maalumu.
Ukaguzi huo umebaini nyaraka za Sh968 milioni kwa wilaya zote na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na wilaya za Same, Hai na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hazikuweza kupatikana kwa ukaguzi.
Malipo ya posho hewa
Ripoti hiyo inasema Sh1.2 bilioni zililipwa kama posho kwa kutumia nyaraka za kugushi na kwamba, mahojiano yaliyofanywa na timu ya ukaguzi maalumu yalibaini kuwa walioonekana kulipwa posho ni wasimamizi wa vituo, lakini baadhi ya waganga wakuu wa wilaya hawayatambui malipo hayo.
Pia, kwa baadhi ya halmashauri waganga wakuu wa wilaya na maofisa utumishi waliyakana majina ya waliolipwa katika fomu hizo kuwa, si watumishi wa halmashauri zao.
Vilevile, ukaguzi huo ulibaini kuwa Sh293 milioni zililipwa kwa watu ambao hawakuhusika katika kazi ya chanjo.
“Ukaguzi wa kina ulibaini kuwa waliolipwa hawakuwa watumishi wa halmashauri husika, wala hawakuweza kujulikana kada zao mahali pao pa kazi,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Hata baada ya timu ya ukaguzi kufanya juhudi za kuwajua ni kina nani na mahali walipo, hawakuweza kupatikana.
Pia, inasema timu ya ukaguzi maalumu ilibaini kuwapo kwa watumishi waliohusika moja kwa moja katika utoaji chanjo ya Surua-Rubella lakini hawakulipwa Sh82 milioni licha ya bajeti kwa ajili ya malipo yao kuwapo.
“Waathirika katika kadhia hii kwa asilimia kubwa, walikuwa ni madereva na watendaji wa kata. Na waliahidiwa wangelipwa iwapo fedha zingekuja, lakini hadi wakati wa ukaguzi huu walikuwa hawajalipwa,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Malipo ya huduma hewa ya chakula
Ukaguzi huo ulibaini nyaraka za matumizi ya Sh316 milioni zinazohusiana na huduma ya chakula ambayo haikutolewa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyaraka hizo zilikuwa ni za kugushi na zilikataliwa na watoa huduma wenyewe kwa maelezo kuwa hazikuwa zao au hawakuziandika wao.
“Ukaguzi ulibaini kuwa, nyaraka hizo zilikuwa za kugushi kutokana na kuwapo kwa kasoro mbalimbali ikiwamo mihuri iliyotumika kutofautiana na mihuri halisi tuliyoipata kutoka kwa watoa huduma hao,” inasema ripoti hiyo.
Pia, saini zilizotumika kwenye nyaraka hizo hazifanani na saini halisi zinazotumika kwenye vitabu vya wazabuni hao na muonekano halisi wa nyaraka za mzabuni unatofautiana na ule wa hati zilizoambatanishwa kwenye marejesho ya matumizi.
Ukaguzi huo umebaini kuwa, baadhi ya nyaraka za kugushi zinamtambua Katibu Mkuu Wizara ya Afya kama mhusika aliyepatiwa huduma wakati huduma zikitolewa katika halmashauri.
Udanganyifu kwenye mafuta
Ripoti hiyo inasema mafuta yenye thamani ya Sh248 milioni yalionekana kununuliwa kwa ajili ya shughuli za chanjo.
Hata hivyo, madaftari ya kuratibu safari za magari yaliyopewa mafuta hayo yamebainisha kuwapo kwa taarifa zisizo na uwiano, hivyo kubainisha kuwa mafuta hayo yalitolewa kwa udanganyifu kutokana na kutokuwapo kwa mtiririko wa namba za stakabadhi.
“Stakabadhi hizo zimepewa namba tofauti na mtiririko wa tarehe husika. Mahojiano na baadhi ya madereva yamebainisha kwamba, mafuta hayo hayakuwa halali na katika maelezo yao wamekana kuyatambua mafuta ambayo yanasemekana kutumika kwenye magari yao,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Madaftari ya kuratibu safari za magari hayakujazwa kwa usahihi, kwani hayakuwa na taarifa ya jina la ofisa aliyekuwa anatumia gari, kiwango cha mafuta yaliyotumika, mahali gari lilipokwenda wala shughuli ya safari hiyo.
Pia, inasema Sh372 milioni zilitumika kulipia mafuta wakati wa chanjo ya Surua Rubella katika mamlaka za serikali za mitaa 55.
Hata hivyo, baada ya ufuatiliaji wa matumizi ya mafuta hayo ilibainika kuwa mafuta yote hayakuingizwa kwenye leja ya mafuta, hivyo kutoweza kuthibitisha matumizi halisi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni kinyume na agizo la 54 (3) la Memoranda ya Fedha ya Serikali za Mtaa ya mwaka 2009.
Pia, ripoti imebaini kuwa vitengo vya ununuzi vya halmashauri husika havikuwa na taarifa yoyote kuhusiana na ununuzi wa mafuta hayo na havikuhusishwa hata kidogo katika mchakato huo.
Matengenezo ya magari
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukaguzi huo ulibaini kuwa Sh137.7 milioni zilitumika kwa ajili ya kutengeneza magari mbalimbali yaliyotumika katika chanjo.
Hata hivyo, uhalali wa matengenezo hayo haukuweza kuthibitishwa kwani baadhi ya karakana hazikuwamo kwenye orodha ya karakana zilizoteuliwa kufanya matengenezo hayo.
Kufuatia kubaini madudu hayo, CAG anashauri mfumo wa udhibiti wa ndani uimarishwe ili kuhakikisha kuwa malipo ya huduma yanafanyika tu pale huduma inapokuwa imetolewa.
Pia, alipendekeza hatua za nidhamu na sheria zichukuliwe dhidi ya wahusika waliotajwa kufanya marejesho ya matumizi kwa kutumia nyaraka za wazabuni za kugushi na kiwango cha fedha kilicholipwa kwa huduma isiyotolewa kirejeshwe na wahusika waliotajwa.
Tupia Comments: