TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI

1. Maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa Chama cha ACT Wazalendo:

Tarehe 05 Mei 2017, Chama cha ACT Wazalendo kitatimiza miaka mitatu tangu kilipopata usajili wa kudumu tarehe 05 Mei 2014 wakati huo kikiitwa ACT Tanzania.
Maadhimisho ya miaka mitatu ya kuzaliwa kwa ACT Wazalendo yatafanyika Kahama Mjini Mkoani Shinyanga tarehe 05 Mei 2017.

Kwa kuzingatia falsafa ya Mpango Mkakati wa Chama ya Siasa ni Maendeleo, maadhimisho ya miaka mitatu ya Chama yatajumuisha shughuli mbalimbali za kijamii kama vile usafi kwenye masoko ya mji,hospitali pamoja na kuwatembelea wafungwa.

Viongozi wa Chama wa kitaifa na mkoa wa Kahama watashiriki kwenye shughuli hizi.
Wanachama, wapenzi na wananchi kwa ujumla mnakaribishwa kwenye sherehe hizi za maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama chetu cha kizalendo.

Maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama yatafuatiwa na mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama kuhusu Itikadi, Oganaizesheni na Usimamizi wa Rasilimali Fedha yatayofanyika tarehe 6 Mei hadi tarehe 7 Mei 2017.

2. Sakata la Wafanyakazi Hewa.
Juzi tarehe 27 Aprili 2017, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) . Angela Kairuki alikabidhi rasmi Ripoti ya Uhakiki wa Vyeti ambapo iliripotiwa kuwa jumla ya watumishi 9932 wanatumia vyeti feki.

Chama cha ACT Wazalendo kinaunga mkono uamuzi wa serikali kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma waliobainika kutumia vyeti feki ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Bila shaka hatua hii itapanda mbegu ya uwajibikaji, kuchochea uadilifu na kuhakikisha uweledi kwenye utumishi wa umma.

Mbali na kupongeza, yapo masuala kadhaa yaliyoibuka kwenye zoezi hilo ambayo tunaamini hayakwenda sawasawa na hivyo basi sisi kwa nafasi yetu tunao wajibu wa kuyakemea ili kuufanya mchakato huu uende kwa haki:

Mosi, kauli ya Mh. Rais kuwasamehe wale watakaojiondosha kazini wenyewe na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na wale watakaoendelea kubaki kwenye nafasi zao ni kinyume cha sheria na katiba ya nchi.

Kisheria Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu anayetuhumiwa kufanya kosa la jinai iwapo mtu huyo hajafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa.

Madaraka pekee aliyonayo Mh. Rais ni kutoa Msamaha kwa wafungwa wanaotumikia kifungo (President's Prerogative of Mercy) kama alivyofanya hivi karibuni kwenye Sherehe za Muungano.

Iwapo tutaacha hulka ya viongozi kuchukua hatua wapendavyo hata kama kwa kusigina sheria za nchi basi tujue wazi tulipeleka taifa kwenye "Utawala wa Mtu Binafsi" badala ya "Utawala wa Sheria".

Pili, madai ya Waziri Kairuki kuwa mchakato wa uhakiki wa vyeti haujawagusa wanasiasa na wateule wa Rais kwa sababu cheti si sifa ya kupatikana kwao unapotosha mantiki nzima na kuweka upendeleo wa dhahiri. Ikumbukwe kuwa msingi wa jambo hili ni kuhakikisha kuwa taifa linabaki na watumishi wenye sifa.

Waziri Kairuki anasema kuwa sifa pekee ya Kikatiba ya Viongozi wa kisiasa ni kuwa wajue kusoma na kuandika. Jambo ambalo Waziri Kairuki hakutaka kujiuliza ni kuwa iwapo viongozi wa kisiasa watathibitika kughushi vyeti ambalo ni kosa la jinai haitawaondolea sifa yao ya uongozi.

Kama Waziri mwenye dhamana ya utawala bora hakuona kuwa uhakiki wa vyeti kwa viongozi wa kisiasa na wateule wa Rais kama vile Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kungehakikisha kuwa viongozi hao wanakwenda sambamba na viapo na matakwa ya kimaadili?

Uamuzi huu wa kutowagusa viongozi wa kisiasa katika zoezi hili la uhakiki wa vyeti ni ushahidi wa dhahiri kabisa wa jinsi serikali inavyohaha kuwalinda baadhi ya wateule wa Rais na wanasiasa ambao wametuhumiwa na umma kwa makosa ya kughushi vyeti.

ACT Wazalendo tunatoa rai kwa serikali kutanua mawanda ya jambo hili liguse viongozi wa kisiasa wa CCM na vyama vya upinzani.

Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano.
30 Aprili 2017

Tupia Comments: