Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba amewaomba wabunge waridhie hatua zilizochukuliwa na serikali kuwahakikishia usalama wa wananchi wanaoishi maeneo yaliotokea matukio ya mauaji ya askari.
“Mheshimiwa Spika nisingependa kwenda kwenye undani wa kitu gani tunakipanga. Umetoka kuweka vizuri kwamba tunaweza kupata fursa ya kuelezea kwenye kamati halafu ikawa vizuri zaidi,” amesema waziri huyo.
Nchemba amefafanua kuwa tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotoa maelekezo tumeweka utaratibu wa namna ya kuwahakikishia wanachi wanaoishi maeneo yalikotokea mauaji hayo usalama wao pamoja na mali zao.
Spika wa Bunge, Job Ndugai alimkaribisha Waziri wa Mambo ya Ndani iliatoe maelezo kwa wabunge juu ya hatua ambazo serikali inazichukua katika kukabiliana na matukio ya mauaji na usalama wa raia na mali zao.
“Na watu wengine walikuwa wanahoji kwamba wananchi wanakuwaje salama kama askari wenyewe wameweza kushambuliwa,” alieleza waziri.
Katika maelezo yake Waziri amesema: Mimi niwahakikishie kwamba askari wetu wamekutana na ajali hii wakiwa kazini.
Ameliambia bunge kuwa kazi waliokuwa wakifanya askari hao ni ya kuhakikisha kwamba raia pamoja na mali zoa zinabakia salama.
“Ni katika mkakati wetu kuwaepusha askari na hatari kama hizi na kuhakikisha kuwa tunakomesha uhalifu huo unaowakabili raia wetu pamoja na askari wenyewe,” ameeleza Nchemba.
Waziri huyo aliwataka wabunge pamoja na kuguswa kwao waridhie hatua ambazo tayari zimechukuliwa na serikali.
Serikali inalichukulia jambo hili kwa uzito mkubwa na kwa utofauti mkubwa kuweza kuhakikisha inarejesha hali ya kawaida katika maeneo ambayo uhalifu umekuwa ukijitokeza na kujirudiarudia, amesisitiza Waziri Nchemba.
Hivi karibuni jeshi la polisi nchini Tanzania liliwauwa watu wanne wanaosadikiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi zaidi ya kumi katika eneo la Mkengeni, kata ya Mjawa, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Pia imetangaza uperesheni maalum katika eneo la Kibiti.
Jeshi la Polisi pia lilitoa maelezo juu ya sababu ya kuwepo mauaji ya askari katika maeneo ya Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na Kibiti.
Limeeleza kuwa ni kwa sababu ya kuwepo mapori makubwa ambayo hutoa mwanya kwa watu wenye naia mbaya ya kutenda vitendo vya uhalifu kupata mahali pa kujificha.
Kamshina wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Msanzya alisema jeshi hilo limeanzisha msako mkali baada ya vitendo vya mauaji hayo ya kinyama Alhamisi na itaendeleza operesheni maalum katika eneo la Kibiti.
Aliongeza kusema kuwa katika mapambano na majambazi hao polisi wamefanikiwa kuzikamata silaha mbili kati ya saba zilizokuwa zimechukuliwa kutoka kwa askari waliouawa, zoezi ambalo lilifanyika katika eneo ambalo mauaji hayo yalifanyika.
Kamanda huyo amesema kuwa katika operesheni hiyo, ambapo kikundi cha upelelezi kilipelekwa mara moja katika eneo la tukio wapelelezi waliweza kugundua maficho ya muda ya majambazi hao na katika kutupiana risasi majambazi wanne waliuawa, aliongeza kusema.

Tupia Comments: