MCHUNGAJI David Mabushi wa Kanisa la IEACT lililopo katika Manispaa ya Shinyanga, amesema kanisa linamuunga mkono Rais John Magufuli kwa yale anayoyatekeleza kulinda rasilimali za umma, huku akimfananisha kiongozi mkuu huyo wa nchi na Nabii Musa, aliyekuja kuwakomboa wana wa Israel.

Mchungaji Mabushi alisema hayo juzi ofisini kwake wakati akizungumza na gazeti hili baada ya kumalizika kwa ibada ya Sikukuu ya Pasaka, huku akieleza kuwa Rais Magufuli amedhamiria kuyafanya aliyokuwa akiahidi katika kipindi cha kampeni wakati wa Uchanguzi Mkuu mwaka 2015 hata Watanzania wakamwamini na kumchagua kuliongoza taifa.

Mabushi alisema kanisa lake linamuunga mkono Rais Magufuli kwa juhudi na kazi zote, anazozifanya kulinda rasilimali za nchi hii zisizidi kuwanufaisha Watanzania wachache. Kiongozi huyo wa dini, alisema utekelezaji wa ahadi alizotoa Rais Magufuli wakati akigombea wadhifa huo pamoja na hatua anazochukua kiutendaji ni mambo yanayoleta tija na ukombozi kwa Watanzania, kama Nabii Musa alivyokuja kuwakomboa wana wa Israel.

Alisema miongoni mwa masuala yaliyokuwa yakilalamikiwa na Watanzania wengi ni pamoja na kuwepo kwa mikataba mibovu ya migodi na mchanga, kusombwa kupelekwa nje ya nchi ukiwa na rasilimali nyingi. Hivyo, alisema kitendo cha kuzuia usafirishaji wa mchanga huo na kuunda tume mbili za kuchunguza ili kujiridhisha kuhusu vilivyomo katika mchanga huo ni cha kijasiri, kwani kimelenga kujiridhisha na hali halisi, na kuondoa manung’uniko kwa kuwa ukweli utakuwa wazi.

“Lakini ninashangazwa na baadhi ya Watanzania wamekuwa kama anachokifanya Rais kukemea uovu, ubadhirifu ufisadi na rushwa sio walichokuwa wakikisema kipindi cha nyuma…Wengi hawataki kupaza sauti kumuunga mkono na sasa sisi tunamuombea kwa Mungu huku tukimshauri amuachie Mungu kila jambo kwa kuwa ameamua kuwatumikia wananchi wanaonyonywa rasilimali zao,” alisema Mchungaji Mabushi.

Tupia Comments: