Milio ya magari ya polisi na magari ya kubebea wagonjwa ilisikika katika mtaa wa Champs Elysees uliopo Paris. Champs Elysees ni mtaa wenye maduka mengi ya kifahari, unapendwa sana na watalii na uko karibu na kasri la Rais wa Ufaransa. Hapo Alhamisi, mida ya saa tatu usiku, mwanaume mmoja alianza kulifyatulia risasi gari la polisi ambapo alimuua afisa mmoja na kuwajeruhi wengine wawili. Polisi walijibu mashambulizi na hatimaye kumuua mshambuliaji huyo.
Awali, kundi linalojiita Dola la Kiislamu lilidai kuhusika na shambulio hilo. Tamko lililosambazwa na shirika la habari la kundi hilo la kigaidi, linasema aliyemuua polisi anaitwa Abu Yousif al-Belgiki, ikimaanisha Mbelgiji kwa Kiarabu. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ubelgiji, Jan Jambon, amesema kwa mujibu wa taarifa walizonazo, mshambuliaji alikuwa raia wa Ufaransa.
Usalama kuimarishwa kabla ya uchaguzi
Jumapili Wafaransa watapiga kura katika duru ya kwanza ya kumchagua rais. Shambulio la Alhamisi usiku limewaweka watu katika hali ya wasiwasi, wakihofia kuwa mashambulio mengine yanaweza kutokea hata siku ya uchaguzi. Waziri Mkuu wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve amesema wanafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuzuia matukio mengine ya aina hii: "Nawakumbusha kuwa serikali imeongeza maafisa wa usalama katika miezi kadhaa iliyopita ili kuhakikisha usalama wa wananchi wetu nchini kote. Katika siku zinazokuja, zaidi ya maafisa wa polisi 50,000 watakuwa kazini kuhakikisha usalama wa mchakato wa uchaguzi."
Shambulio la mtaa wa Champs Elysees lilifanyika wakati wagombea wa urais walipokuwa kwenye mdahalo wa televisheni, wakinadi sera zao kwa wapiga kura. Marine Le Pen, mgombea wa chama chenye siasa za kupinga uhamiaji, Front National, aliitumia fursa hiyo kurudia msimamo wake:
"Nataka tuwe na mkakati wa kupambana na ugaidi wa Waislamu wenye itikadi kali. Tunapaswa kuung'oa mzizi wa uovu huu. Naamanisha itikadi hii ambayo imekuwa ikiongezeka nchini mwetu kwa miaka mingi."
Aidha, Le Pen ametaka utaratibu wa kukagua watu wanapovuka mpaka kuingia Ufaransa urejeshwe. Mgombea wa kujitegemea Emmanuel Macron, anayeongoza maoni ya wapiga kura, amewataka Wafaransa wawe watulivu, akikumbusha kwamba magaidi wana nia ya kutetemesha demokrasia nchini. Naye Rais Francois Hollande ameitisha kikao cha dharura cha baraza la usalama la serikali kujadili tukio la jana.
Tupia Comments: