SERIKALI ya Marekani imesema itaendelea kutoa misaada ya kiuchumi, ustawi wa jamii na kisiasa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ili kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.
Msimamo huo umeelezwa katika ziara ya ujumbe wa Serikali ya Marekani uliotembelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya sera za kiuchumi, kisiasa na kijamii huko Ofisi Kuu Kisiwandui Unguja.
Marekani ambayo ni Taifa kubwa lililoendelea kiuchumi, kijamii na kiulinzi, imesema kasi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Saba Zanzibar, linaishawishi taifa hilo kutoa misaada binafsi na inayopitia katika ngazi za kimataifa, ili kuenzi kwa vitendo juhudi hizo.
Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Ofisa wa kusimamia Masuala ya Sera za Kijamii na Kisiasa katika Ukanda wa Nchi za Afrika zilizomo katika Jangwa la Sahara, Gregory Simpkims alieleza kwamba CCM iimekomaa kisiasa na inaendelea kuimarika, tofauti na vyama vya kisiasa vya nchi nyingine barani Afrika, ambavyo baadhi yao vimeanza kupoteza nguvu na kuondolewa madakarani na vyama vya upinzani.
“Pia tunaamini kuwa vyama vya siasa vilivyopo Zanzibar vitaendelea kulinda amani ya visiwa vya Zanzibar ili viwe sehemu tulivu inayoshawishi kila taifa kufanya utalii na shughuli nyingine za kijamii.”
Pia ujumbe huo ulitaka kujua njia na sera zinazotumiwa na CCM kuendelea kuaminiwa na wananchi wa Tanzania na Zanzibar, hali inayosababisha kuimarika kwa uchumi wa nchi hiyo.
Alisema kwamba ujumbe huo ulitaka kujua mambo mbalimbali yakiwemo suala la Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, siri ya kuimarika kwa CCM kisiasa na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi wa Taifa la Marekani na sera za nchi za nje za taifa hilo kwa upande wa Zanzibar.
Alisema walizungumzia uimarishaji wa sera za kibiashara na kiuchumi ya nchi za Afrika, ambayo ni Mpango wa Fursa za Kiuchumi za Afrika nchini Marekani (AGOA), na kueleza kuwa kwa sasa wapo tayari Zanzibar kunufaika na mpango huo ili bidhaa zake zikauzwe katika soko hilo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma Saadalla maarufu kama Mabodi, alisema ujumbe huo ulihoji kwa nini taarifa ya wasimamizi wa kimataifa wa uchaguzi wa mwaka 2015, ilikuwa tofauti na taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Alifafanua kwamba jawabu la swali hilo, lilikuwa ni kwamba CCM inaamini na kuunga mkono taarifa na maelekezo ya Tume hiyo, kwani ndio iliyokuwa ikisimamia shughuli za uchaguzi tangu awali.
Tupia Comments: