Uhakiki wa vyeti uliofanywa na ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora haujawagusa viongozi wa kisiasa ambao wako serikalini kama vile mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya.
“ Uhakiki huu haujafanyika kwa viongozi wa kisiasa ambao wako serikalini kama vile Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao mamlaka ya uteuzi ndio wanajua ufanisi wa kazi zao na pia katika siasa suala ni kujua kusoma na kuandika.” Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amefafanua.
Lakini hata hivyo waziri amesema watumishi wa umma wataajiriwa kulingana na sifa zilizoainishwa kwenye miongozo mbalimbali.
Amesema uhakiki wa vyeti uliofanyika ni wa kidato cha nne na sita na vyeti vya ualimu na diploma. Amesema uhakiki huo ulifanyika kwa watumishi wa serikali za mitaa, mashirika ya umma, wakala wa serikali, serikali kuu, wizara na idara zinazojitegemea.
Amesema kati ya vyeti 1,114 vilivyowasilishwa Baraza la Mitihani kwa uhakiki, vyeti 344 vilikuwa vikifanana na watumishi hao walichukuliwa hatua kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa mujibu wa repoti hiyo aliyokabidhiwa Rais matokeo ya uhakiki kundi la kwanza; watumishi 376,969 sawa na asilimia 94.3 walikuwa na vyeti halali na Baraza la Mitihani limejiridhisha magamba ya vyeti yaliyohakikiwa yalitolewa na baraza hilo.
Alisema watumishi 9,932 sawa na asilimia 2.4 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi kutokana na miundo ya vyeti vyao kutofanana na vyeti husika. Pia watumishi wenye vyeti vyenye utata vilivyohakikiwa ni 1,538 sawa na asilimia 0.3.
Kairuki amesema watumishi 11,566 sawa na asilimia 2.8 waliwasilisha vyeti vya utaalamu peke yake bila cheti cha kidato cha nne au cha sita na wanafuatilia kwa makini ili kujua mwisho wake. “Suala la kughushi ni kosa la jinai na hatua zitachukuliwa kwa mawakala wanaotengeneza vyeti vya kughushi.”
Amesema katika sheria za nchi adhabu za mtu anayeghushi cheti ni kifungo cha miaka mitano gerezani. Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema kumekuwa na changamoto kubwa ya kughushi vyeti vya taaluma au kutumia vyeti vya watu wengine.
Amesema mwaka 2008 ulianzishwa utaratibu wa kuweka picha kwenye vyeti na kuliongezeka maficho yanayowekwa kwenye vyeti vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.
Tupia Comments: