Kampuni ya simu TTCL yaja kivingine


KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imetumia vyema Jukwaa la Biashara mkoani Mwanza kueleza mikakati yake madhubuti ambayo inaifanya kuwa tegemeo kwa wateja wengi hususani wawekezaji na wafanyabiashara.
Kampuni hiyo ilianza kwa kugawa bure huduma ya mtandao kwa njia ya ‘wifi’ kwa washiriki takribani 300 waliohudhuria jukwaa hilo katika ukumbi wa Rockcity Mall.
Wengi, baadhi yao wakiwemo waandishi wa habari waliokuwa na kompyuta mpakato walishangaa kasi kubwa ya 4G LTE ya TCCL.
Wakati watu wakistaajabu kasi hiyo, Mkuu wa kitengo cha Biashara wa TTCL, Kanda ya Ziwa, Karim Bablia alisema kasi walioishuhudia washiriki wa jukwaa bado siyo yenyewe kutokana na tatizo lililoko kwenye mkongo wa taifa.
Bablia alisema TTCL pia inatoa huduma bora ya simu kwa kutumia simu za mkononi (mobile network) na ya kawaida (fixed network) na kuwataka watu wajaribu waone ‘maajabu’.
Alisema wanatoa pia huduma za takwimu na video pia wanatoa huduma kwa ajili watumiaji wengine wa mitandao au huduma ya kuunganisha matawi mbalimbali.
Alisema watu wengi wasichojua ni kwamba benki nyingi nchini na taasisi kama Tamisemi zimeungwa na mtandao wa TTCL.
“Tuna huduma nyingi sana Mwenyekiti (Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella), na hivyo ni vyema mwekezaji yeyote anayekuja Mwanza (na miji mingine nchini) atuone TTCL kwani atapata huduma bora kabisa ambazo hawezi kuzipata kwingineko,” alisema.
Alisema kuna hoteli kadhaa zikiwemo zilizoko kwenye mbuga za wanyama ambazo wamezipa huduma ya intaneti kwa majaribio na wanakiri kwamba hawajawahi kupata huduma bora kama hiyo.
“Naona kuna wengine hapa ukumbini tuliowapa huduma zetu. Kama kuna asiyeamini anaweza kuwauliza,” alisema na kuongeza kwamba yeyote anayetaka kujaribu huduma zao, TTCL Mwanza iko tayari kutoa huduma ya majaribio kwa siku 14 bure.
Bablia alisema kampuni yao inatangaza fursa lukuki za biashara kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara.
“Tunatoa fursa ya uuzaji wa vifaa vya vya mawasiliano kama vile modem, laini za simu na kadhalika. Njoo TTCL nitakupa hivi vifaa. Hii ni fursa.”
Alisema kuna kadi zao za TTCL, kwa kila wakala atakayenunua kadi ya Sh 500, ataiuza kwa mteja kwa shilingi 2000, na kupata faida ya 1,500.
“Faida zilizomo kwenye kadi hii ni mazungumzo kwa simu za TTCL bure kwa mwezi mzima, sms (ujumbe wa simu) 200 na MB 200 bure,” alisema.
Alisema TTCL pia inasimamia kituo cha takwimu cha taifa ambacho ni kitovu cha uwekezaji. Kadhalika akasema TTCL inayo majengo ya kukodisha kwani wametoka kwenye teknolojia iliyotaka majengo makubwa hadi madogo na hivyo kubaki na nafasi za kutosha.
“Tuna huduma pia ya kuweka mitambo ya mawasiliano. Jamani IT siyo simu tu bali hata huduma zingine za kibenki na kwamba mtu akiweka mitambo yake TTCL atakuwa na uhakika wa mambo mengi ikiwamo umeme wa uhakika,” alisema.
Alizikumbusha taasisi zinazohitaji bando kubwa katika matumizi yao zikiwemo za serikali zisihangaike kwenda kununua kwingineko bali TTCL kwani ni bei rahisi.
Bablia alisema kampuni yao pia ina mikakati ya kuleta huduma ya kutoa na kuweka pesa (mobile money) ambapo katika huduma hiyo watahitajika mawakala wa kutosha kwa ajili ya uenezaji wa huduma hiyo itakayokuwa na nafuu kuliko ‘wengine’.
Katika hatua nyingine, Bablia alisema mtu yeyote atakayemtaja au kumripoti mtu anayeiba mali za kampuni ya simu (TTCL) atazawadiwa shilingi 300,000.
Bablia alisema wezi wamekuwa wakiiba mali za kampuni yao kama nguzo na mifuniko ya chuma na kadhalika.
“Pia tunatafuta wakala ambae atatusaidia katika ukusanyaji wa madeni yetu kwa wadaiwa wetu,’’ alisema.
Jukwaa la Biashara Mwanza liliandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha HabariLeo, Daily News na SpotiLeo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Mbali na TTCL, wadau wengine walitoa elimu muhimu kwa wafanyabiashara wa Mwanza ni mabenki ya NMB, TIB (Development), TIB (Corporate) na Benki ya TPB.
Wadau wengine waliotoa mada zao juzi ni Bohari ya Dawa (MSD), hoteli ya kisasa jijini Mwanza ya Victoria Palace, Mamlaka ya Mapato (TRA), Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na Watumishi Housing Company (WHC).

Tupia Comments: