Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli leo Sikukuu ya Pasaka, wameungana na Waumini wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni kusali Ibada ya Pasaka.
Katika Ibada hiyo Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba Askofu Charles Salalah ameongoza maombi ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na amempongeza kwa kazi kubwa ya kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya na kufuja mali za umma.
“Mhe. Rais unafanya kazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua wewe ni majipu madogomadogo yaliyotokana na jipu kuu ambalo ni dhambi za mwanadamu, na jipu hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu, kwa hiyo sisi Wakristo wenzako na waumini wengine tunakuombea sana na tunakuunga mkono katika kazi hii nzito ya kutumbua majipu haya madogomadogo ya watumishi hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na mengine mengi” amesema Askofu Charles Salalah.
Akizungumza katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Wakristo wa Kanisa la Africa Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa kuendelea kumuombea na ameomba maombi hayo yaendelee, na piawaiombee nchi iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.
Mapema asubuhi Mhe. Rais Magufuli ameshiriki Ibada ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo katika Parokia ya Oysterbay Jijini Dar es Salaam ambapo katika salamu zake za Pasaka Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengoamesema baraka zilizoletwa na Yesu Kristo aliyefufuka ni kwa ajili ya watu wote wakristo na wasio wakristo na amemtakia heri Mhe. Rais Magufuli ili matumaini ya baraka hizo ziwafikie Watanzania wote.
Amemuombea Mhe. Rais Magufuli kuwa imara katika changamoto na machungu anayokutana nayo katika uongozi akisema “Yesu Kritso akuimarishe na akutie nguvu ili matumaini tunayoyadhimisha leo yawafikie Watanzania wote”
Tupia Comments: