TPA, TICTS wasaini mkataba mpya, Majadiliano yachukua miezi 7 kufikia muafaka.

Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania TPA na kampuni ya kimataifa ya kuhudumia makasha Tanzania TICTS zimesaini mkataba mpya baada ya majadiliano yaliyochukua miezi saba kufikiwa kwa makubaliano.

Akizungumza katika hafla hiyo waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema mkataba huu mpya umeondoa masharti hasi ambayo yalikuwa yanabana maslahi kwa Tanzania, ambapo kwa sasa TICTS watalipa kodi ya mwaka ya dola milioni 14 kutoka dola milioni saba za kwenye mkataba wa awali, kodi ambayo itakuwa ikiongezeka kwa asilimia tatu kila mwaka.

Vile vile kodi ya makasha itakuwa dola ishirini kutoka dola kumi na tatu za kwenye mkataba wa awali ambayo pia itakuwa ikiongezeka kila mwaka kwa asilimia 4.

800x800_560ccc8b7a464.jpg

Kwa upande wake waziri wa katiba na sheria Profesa Paramagamba Kabudi, ambaye ameshuhudia utiwaji saini wa mkataba huo mpya, amesema mkataba huu ni miongoni mwa mikataba iliyosaidia kujua kwamba kuna umuhimu wa kupitiwa kwa mikataba mingi ambayo imeonekana kutokuwa na manufaa kwa Tanzania na kutoa rai kwa wenye dhamana nchini.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya agizo la rais Dkt John Pombe Magufuli alipotembelea bandari ya Dar es Salaam na kutaka kupitiwa kwa mkataba huo wa TPA na TICTS. Aidha mkataba huu unasainiwa huku Bunge likiwa limepitisha sheria ya kupitia mikataba yote yenye masharti hasi, sheria ambayo inasubiri kusainiwa na Raisi ili kuanza kufanya kazi.

Tupia Comments: