Mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi, G20 unaanza kesho mjini Hamburg, Ujerumani, huku maelfu ya watu wakiandamana kuupinga mkutano huo.
Mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi, G20 unaanza kesho mjini Hamburg, Ujerumani, huku maelfu ya watu wakiandamana kuupinga mkutano huo.
Kiasi ya waandamanaji 100,000 wanatarajia kushiriki katika maandamano ya leo yaliyopewa jina ''G20: Karibu Jehanamu,'' huku vikosi vya usalama vikisema kuwa kiasi ya waandamanaji 8,000 wanaonekana wako tayari kufanya ghasia na hivyo kutoa changamoto kubwa kwa maafisa wa usalama waliopangiwa kazi ya kuwalinda viongozi wa G20.
Mkuu wa polisi wa Hamburg, Ralf Martin amesema maandamano yaliyofanyika mpaka sasa yamefanyika kwa utulivu mkubwa, ingawa wana wasiwasi kama maandamano ya leo yataendelea kuwa ya amani.
Wanaharakati hao walioapa kuuvuruga mkutano huo wa siku mbili wa G20 utakaoanza kesho Ijumaa, wamebeba mabango yaliyoandikwa ''Bora nicheze dansi kuliko G20.'' Kiasi ya maafisa 20,000 wa usalama wanafanya doria katika mji huo.
Mbali na maandamano pia mkutano wa G20 utatawaliwa na ajenda kadhaa likiwemo suala la mabadiliko ya tabia nchi, usalama pamoja na biashara ya kimataifa. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo wa G20, amesema mkutano huo utafanyika chini ya hali ngumu zaidi ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kama vile ugaidi, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ulinzi na kwamba yote hayo yatajadiliwa.
Dunia haijaungana
Merkel amesema dunia iko katika hali ya machafuko na haijaungana. Ukosefu wa umoja umewahusisha Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Urusi Vladmir Putin na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Viongozi wote hao watatu watahudhuria mkutano wa G20 na tayari kila mmoja ana ajenda yake. Baadae leo, Erdogan atakutana na Kansela Merkel mjini Berlin.
Trump anataka kutumia fursa ya mkutano huo kukutana na Putin ana kwa ana kwa mara ya kwanza, ambapo watakuwa na mambo mengi ya kujadiliana, kuanzia mzozo wa Ukraine hadi vita vya Syria, vikwazo dhidi ya Urusi na madai ya ushawishi wa Urusi katika uchaguzi mkuu uliopita wa Marekani.
Hata hivyo, Trump ameipongeza Poland kwa mchango wake katika usalama wa Ulaya na dunia. Kauli hiyo ameitoa leo mjini Warsaw, Poland katika mkutano wa pamoja na Rais wa Poland, Andrzej Duda na waandishi habari.
''Sio tu lazima tuhakikishe usalama wa mataifa yetu kutokana na kitisho cha ugaidi, lakini tunapaswa pia kukabiliana na kitisho cha Korea Kaskazini. Mimi na Rais Duda tunazisihi nchi zote kupambana na kitisho cha dunia na kupinga wazi wazi kile ambacho Korea Kaskazini inafanya kwani itawajibishwa kutokana na tabia yake hiyo mbaya,'' alisema Trump.
Trump pia amesema anashirikiana na Poland kuelezea vitisho vya Urusi na amerudia wito wake kuzitaka nchi wanachama wa Jumuia ya kujihami ya NATO kutimiza majukumu yao ya kuchangia fedha. Trump yuko Poland kukutana na wakuu wa nchi za Ulaya ya Kati, nchi za Balkan na eneo la Baltic. Kabla ya ziara hiyo, Rais Duda alisema ziara ya Trump itaongeza hadhi ya Poland katika Umoja wa Ulaya.
Tupia Comments: