Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Borge Brende amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Norway itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania hususani kuboresha huduma za kijamii na uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Mhe. Borge Brende aliyeongozana na Balozi wa Norway hapa nchini Mhe. Hanne-Marie Kaarstad amesema hayo leo tarehe 30 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Borge Brende amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kupambana na rushwa, kukabiliana na matumizi mabaya ya ofisi za umma na kusimamia vizuri uchumi na shughuli za maendeleo na kwamba Norway inavutiwa na juhudi hizo na ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano kuimarisha zaidi juhudi hizo.
“Uhusiano wa Tanzania na Norway umedumu kwa miaka 55 na tumeshirikiana katika mambo mengi yakiwemo kuendeleza elimu na miundombinu mbalimbali na sasa tunatarajia kushirikiana zaidi na Tanzania kwa kuwekeza katika miradi mikubwa kama vile uzalishaji wa umeme, kuchakata gesi na kuzalisha mbolea” amesema Mhe. Borge Brende.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Norway kwa mchango wake mkubwa ilioutoa kwa Tanzania tangu uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi uanze na amesema Serikali ya Awamu ya Tano inakaribisha ushirikiano zaidi na Norway hasa uwekezaji utakaokuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
“Hivi sasa tumedhamiria kujenga mradi wa kuzalishaji umeme kwa kutumia maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), lakini pia nchi yetu ina vyanzo vingine vya kuzalisha umeme kama vile maporomoko ya maji katika mito mingine, gesi ambayo mpaka sasa tumegundua futi za ujazo zaidi ya Trilioni 57, tuna makaa ya mawe, jua na upepo mwingi kwa ajili ya kuzalisha umeme, kwa hiyo tunawakaribisha wawekezaji kutoka Norway tushirikiane kuwekeza kwenye maeneo hayo” Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Tupia Comments: