WAISLAMU nchini Tanzania leo wanaungana na wengine duniani kusherehekea Sikukuu ya Idd el fitri baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na visiwani hapa, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anatazamiwa kuwa mgeni rasmi katika sala pamoja na Baraza la Idd kwenye Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Wakfu na Mali ya Amana, imesema sala ya Idd itaswaliwa kwenye Viwanja vya Maisara na kama kutakuwa na mazingira ya mvua itafanyika kwenye Msikiti wa Muembe. Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo, imesema maandalizi ya sala ya Idd pamoja na Baraza la Idd yamekamilika ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa na serikali pamoja na wananchi wa kawaida.
Waislamu wanasherehekea Sikukuu ya Idd kutokana na kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambayo ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu. Waumini wa dini ya Kiislamu wamekuwa katika harakati kubwa za maadhimisho ya sherehe hizo kwa kutaafuta nguo ikiwa ni zawadi kwa watoto wao. Aidha, katika maandalizi hayo baadhi ya bidhaa zikipanda kwa bei kubwa ikiwemo mayai ambayo ni maarufu wa ajili ya kutengeneza keki na vitafunio mbalimbali.
Zanzibar imekumbwa na upungufu wa mayai katika kipindi hiki cha maandalizi ya Sikukuu ya Idd na kulazimika kutegemea bidhaa hiyo kutoka Tanzania Bara na kisiwa cha Pemba. “Mayai hapa hayapatikani tulikuwa na matarajio kuingia kutoka Pemba kwa meli ya Azam Marine na mengine tunayatarajio kutoka Bara,” alieleza mfanyabiashara maarufu wa mayai, Idd Juma. Yai moja moja limekuwa likiuzwa kati ya Sh 500 hadi 400 kutoka katika bei ya kawaida Sh 200.
Wakati wananchi wakijitayarisha na Sikukuu ya Idd, Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja imewataka wananchi kuwa watulivu huku ulinzi ukiimarishwa katika sehemu zote muhimu ambazo hutumiwa na wananchi pamoja na watoto. Akitoa salama za sikukuu, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud aliwataka wananchi kusherehekea sikukuu ya Idd kwa amani na mafanikio makubwa na kujiepusha na matukio yatakayopelekea kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
Aidha, alisema amri ya marufuku ya wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa za vyakula vya maji maji ipo pale pale kutokana na kuwepo kwa hatari ya ugonjwa wa kipindupindu. Alisema mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu bado upo ambapo wapo wagonjwa wamelazwa katika kambi ya Chumbuni mjini Unguja na baadhi ya Wilaya za Unguja. Kwa mujibu wa taarifa za Idara ya Afya Kinga, jumla ya wagonjwa 300 walilazwa katika kambi ya Chumbuni Unguja kwa nyakati tofauti huku watu wanne wakifariki dunia.
Tupia Comments: