Gazeti la Washington Post la nchini Marekani limeripoti kuwa Rais Donald Trump anachunguzwa kuhusiana na madai ya kuzuwia uchunguzi juu uwezekano wa Urusi kuingilia kati uchaguzi wa Marekani mwaka uliopita.
Katika mabadiliko makubwa katika uchunguzi huo uliovutia zaidi nadhari ya Wamarekani katika muda wa miongo kadhaa, maafisa wandamizi wa upelelezi wamekubali kuhojiwa na wachunguzi wa tume maalumu ya Robert Mueller, lilisema gazeti la Washington Post.
Gazeti hilo liliwanukuu watu watano walioarifiwa juu ya maombi hayo na kusema waliokubali kuhojiwa ni mkurugenzi wa idara ya taifa ya uchunguzi Daniel Coats, mkuu wa shirika la usalama wa taifa NSA, Admiral Mike Rogers, na naibu wake aliendoka hivi karibuni Richard Ledgett.
Gazeti hilo limesema mahojiano yatafanyika wiki hii. Habari hiyo ya Washington Post ilipokelewa kwa hasira na timu ya mawakili wa Trump, ambapo msemaji wake Mark Corallo, alisema uvujishaji huo wa taarifa kumhusu rais na wafanyakazi wa shirika la FBI unachukiza, hausameheki na ni kinyume cha sheria. Mabadiliko katika uchunguzi huo kuelelekea kwa rais Trump yalianza siku kadhaa baada ya Trump kumfuta kazi Comey kama mkuu wa FBI Mei 9, lilisema gazeti la Post.
Wataalamu wa masuala ya sheria wamesema ushahidi wa Comey wiki iliopita kwamba Trump alitarajia utiifu na kumuambia Comey kuwa alitumai angeachana na uchunguzi dhidi ya msaidizi wake wa zamani Michael Flynn, huenda ukashadidia madai ya uingiliaji wa uchunguzi dhidi ya Trump. Comey hakuweza kusema katika ushahidi wake wiki iliopita, iwapo alidhani rais alitaka kuzuwia uchunguzi huo, lakini aliongeza kuwa itakuwa juu ya Mchunguzi Maalumu Mueller kubainisha hilo.Ushahidi wa Comey wamuweka kitanzini
Baada ya ushahid wa Comey, Trump alisema amethibitishwa kutokuwa na hatia kwa sababu mkurugenzi huyo wa zamani wa FBI alithibitsha kumuambia mara tatu kwamba hakuwa anachunguzwa. Wakati hakuna uwezekano mkubwa kwa rais alieko madarakani kukabiliwa na mashitaka ya uhalifu, kosa la kuzuiwia utekelezaji wa haki linaweza kujenga msingi wa kuanzisha mchakato wa kuondolewa madarakani.
Wamarekani wengi waeleza mashaka yao
Lakini hatua kama hiyo itakabiliwa na kikwazo kikubwa kwa sababu itahitaji kuidhinishwa na bunge, ambalo linadhibitiwa na chama cha Trump cha Repblican. Kufuatia ushahidi wa Comey, uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja na shirika la habari la Associated Press na kituo cha utafiti wa masuala ya umma cha NORC, unaonyesha kuwa asilimia 68 ya Wamarekani wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa Trump au timu yake ya kampeni walikuwa na mahusiano yasiyofaa na Urusi. Karibu nusu ya Wamarekani wote wanasema suala hilo linawahusu pakubwa na watatu kati ya 10 wakisemma haliwahusu.
Wakati huo huo, mtu mwenye silaha alieripotiwa kuwa na hasira dhidi ya Trump na wabunge wa chama cha Republican, aliwafyatulia risasi wabunge wa chama hicho waliokuwa wanafanya mazoezi kujiandaa na mchezo wa hisani wa baseball jimboni Vaginia, na kumjeruhi vibaya mnadhimu wa chama hicho bunge Steve Scalise na watu wengine watatu kabla ya mtu huyo kupigwa risasi na kuuawa na polisi.
Tupia Comments: