UONGOZI wa Yanga upo kwenye hatua za mwisho za kufanikisha kumuongezea mkataba mwingine mshambuliaji wao tegemeo raia wa Burundi, Amissi Tambwe.
Yanga wanamuongezea mkataba Mrundi huyo, baada ya ule wa awali kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.
Wachezaji wengi walio kwenye mazungumzo nao kwa ajili ya kuwaongezea mikataba ni Deus Kaseke, Deogratius Munishi ‘Dida’, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, mshambuliaji huyo juzi alikutana na viongozi na kufikia muafaka mzuri wa kuongeza mkataba huo mpya wa miaka miwili.
“Tambwe ameonyesha nia kubwa ya kubaki kuendelea kuichezea Yanga, ni baada ya mazungumzo mazuri tuliyoyafanya kati yetu viongozi na yeye mchezaji.
“Makubaliano tuliyoyafikia ni kwamba ataongeza mkataba mwingine wa miaka miwili ya kuendelea kuichezea Yanga, hivyo wakati wowote tutamalizana,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa katibu mkuu wa timu hiyo, Boniface Mkwasa, kuzungumzia hilo, alisema: “Ni kweli kabisa Tambwe tulikutana naye juzi (Jumamosi iliyopita) na kikubwa tulijadiliana hatima yake, na amekubali kubaki na tupo kwenye makubaliano mazuri.”
Alipoulizwa Tambwe kuhusiana na suala hilo, alisema:
“Ni kweli nimeshazungumza nao lakini bado kuna baadhi ya mambo hayajakaa sawa na atakapokamilika, basi kila kitu kitakuwa wazi ila ninaamini nitabakia Yanga.”
Tupia Comments: