Rais Ashraf Ghani na Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi.
China imeanza rasmi juhudi za kuleta suluhu ili kupunguza mvutano uliopo kati ya Afghanistan na Pakistan.
Juhudi hizo zinakusudia kuwatia moyo majirani hao wenye wasiwasi, ili wakubaliane kufanya kazi pamoja katika kupambana na ugaidi na kuendeleza amani katika eneo hilo.
Juhudi za Beijing za kidiplomasia zimekuja wakati mahusiano kati ya Islamabad na Kabul yametetereka katika kipindi cha miaka miwili iliopita kutokana na madai ya pande zote mbili kwamba kila upande unasaidia mashambulizi ya magaidi katika ardhi ya mwengine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesafiri kwenda Kabul Jumamosi, ambapo alikutana na Rais Ashraf Ghani na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa Afghan kuzungumzia jinsi ya kuboresha mahusiano yao na Pakistan.
Tamko rasmi la serikali baadae lilimnukuu Yi akiwaambia viongozi katika mazungumzo hayo wa Afghan kuwa “iwapo itahitajika China itakuwa tayari kusimamia na kueleza hatua” ambazo pande zote Pakistan na Afghanistan wanazo zichukuwa dhidi ya ugaidi na siasa kali.
Mapema mwaka huu, hatua za kidiplomasia zilichukuliwa na Uingereza kusaidia kulegeza mivutano kati ya Pakistan na Afghanistan.
Usuluhisho huo ulipelekea kufikia maelewano kwamba nchi hizo mbili zitafute njia ya kutatua mgogoro unaowahusu na kuendeleza juhudi za kutafuta amani.
Ghani baadae alipendekeza kuhusishwa nchi ya tatu ili kusaidia kuthibitisha juhudi hizo zinachukuliwa na nchi mbili hizo na kufikia malengo, jambo lililopelekea China kuchukua nafasi hiyo ya juhudi za kutafuta usuluhishi kwani inamahusiano mazuri na pande zote, Pakistan na Afghanistan.
Tamko lililotolewa na ofisi ya Ghani limemnukuu rais akisema, “Wang anaamini kuwa Pakistan inaushawishi juu ya Taliban na itawataka Pakistan wawadhibiti kwa makini kabisa, hasa kikundi cha Haqqani.
Tamko hilo limeongeza kuwa waziri wa mambo ya nje wa China alisema ataisisitiza kwamba Pakistan ichukue ahadi ya kupambana na ugaidi.
Waziri wa mambo ya nje wa China aliwasili baadae Islamabad kwa ajili ya kuendeleza jukumu lake katika kutafuta suluhu na kufanya mazungumzo na mshauri wa sera za kigeni wa Pakistan Sartaj Aziz. Haikuweza kujulikana mara moja iwapo Yi alikuja na mapendekezo yoyote kutoka upande wa Afghan.
Pande zote mbili zimefanya mazungumzo kwenye masuala mbalimbali na kupitia kwa ufupi masuala yanayohusiana na ushirikiano kati ya nchi hizo, usalama wa eneo na hali halisi ya Afghanistan,” Msemaji wa Wizara wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Nafees Zakaria amesema.
Waziri wa mambo ya nje wa China amepangiwa kukutana na mkuu wa majeshi ya Pakistani General Qamar Javed Bajwa siku ya Jumapili kabla ya kuwa na mkutano wa pamoja na Aziz na waandishi na kuwafahamisha yale yaliojiri katika mazungumzo yao.
Yi atasafari kurejea Kabul ili kuwapa viongozi wa Afghan muhtasari juu ya mikutano yake wakati akiwa Islamabad, maafisa wamesema.
Tupia Comments: