Kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei akipiga kura
Wairan walipiga kura katika uchaguzi wa rais hapo jana,(19.05.2017)uchaguzi ambao ulikuwa na ushindani mkali kati ya mwanasiasa mwenye msimamo wa wastani Hassan Rouhani na mhafidhina mwenye msimamo mkali Ebrahim Raisi.
Zoezi la kuhesabu kura limeanza nchini Iran leo Jumamosi baada ya wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ambao bila kutarajiwa umekuwa wenye mvutano mkubwa baina ya rais wa sasa Hassan Rouhani , ambaye anataka kurejesha mahusiano ya kawaida na mataifa ya magharibi, dhidi ya jaji mwenye msimamo mkali ambaye anasema kwamba rais wa sasa tayari amekwenda mbali mno.
Zaidi ya wapiga kura milioni 40 walipiga kura, imesema wizara ya mambo ya ndani , ikiashiria kwamba watu waliojitokeza wanafikia asilimia 70 katika uchaguzi uliofanyika jana Ijumaa , karibu sawa na jinsi watu walivyojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2013 wakati Rouhani alipoingia madarakani kwa ushindi wa kishindo.
Upigaji kura ulirefushwa kwa masaa sita kwasababu watu wengi bado walikuwa katika mistari. Magazeti nchini Iran yamesifu jinsi watu walivyojitokeza kupiga kura, yakiandika vichwa vya habari kama "ushindi wa kihistoria kwa Wairani".
Kasi ya mabadiliko imekuwa ndogo
Tovuti za habari zinazounga mkono mageuzi zimesema Rouhani alikuwa mshindi. Hata hivyo hawakutoa ushahidi, lakini watu kujitokeza kwa wingi kunaweza kuelemea upande wa Rouhani, ambapo wasi wasi mkubwa wa waungaji wake mkono ni kuchoshwa miongoni mwa wapiga kura wanaopendelea mageuzi waliovunjwa moyo na kasi ndogo ya mabadiliko.
Rouhani , mwenye umri wa miaka 68, ambaye aliingia madarakani akiahidi kuiweka Iran karibu na mataifa ulimwenguni na kuwapa raia wake uhuru zaidi nyumbani , anakabiliana na upinzani mkali bila kutarajia kutoka kwa Ebrahim Raisi mwenye msimamo mkali, anayeungwa mkono na kiongozi mkuu nchini humo Ali Khamenei.
Uchaguzi huo ni muhimu "kwa hali ya baadaye ya jukumu la Iran katika eneo hilo na dunia kwa jumla", Rouhani , ambaye alipata makubaliano na mataifa makubwa yenye nguvu kuiondolea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi, alisema baada ya kupiga kura.
Raisi mwenye umri wa miaka 56 , amemshutumu Rouhani kwa kuuvuruga uchumi wa nchi hiyo na amesafiri hadi katika maeneo wanakoishi masikini, akizungumza katika mikutano akiahidi mafao zaidi ya kijamii na ajira.
Matokeo yataheshimiwa
Anaaminika kuwa anaungwa mkono na majeshi yenye ushawishi mkubwa nchini humo ya walinzi wa mapinduzi, pamoja na uungwaji mkono mkubwa wa kiongozi mkuu nchini humo Khamenei, ambaye madaraka yake yanapindukia yale ya rais aliyechaguliwa ambae lakini kwa kawaida hujiweka mbali na shughuli za kila siku za kisiasa.
"Naheshimu matokeo ya kura za wananchi na matokeo yataheshimiwa nami pamoja na wananchi," Raisi alisema baada ya kupiga kura, kwa mujibu wa shirika lisilokuwa rasmi la habari Fars.
Hata hivyo , Raisi alijitokeza katika wizara ya mambo ya ndani mjini Tehran siku ya Ijumaa na kulalamikia upungufu wa karatasi za kupigia kura katika vituo vingi vya kupigia kura, kwa mujibu wa shirika la habari la Fars. Makaratasi zaidi ya kupigia kura yalipelekwa katika vituo, shirika hilo lilisema.
Tupia Comments: