VIONGOZI wa Kamati ya Utendaji ya Yanga wameigomea barua ya kujizulu waliyoandikiwa na mwenyekiti wao, Yusuf Manji na kumuomba abatilishe uamuzi wake huo ili aendelee kuongoza.
Manji, Jumanne iliyopita aliandika barua ya kujiondoa nafasi hiyo huku akitaja sababu kubwa ni kuwapisha watu wengine wapya waiongoze timu hiyo kwa mafanikio.
Wakati anaaga kuondoka, siku hiyohiyo Wenyeviti wa Matawi ya Yanga, haraka walikutana kwenye makao makuu ya klabu hiyo kwa ajili ya kupinga uamuzi huo wa Manji.
Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga aliliambia Championi Jumamoi kuwa, juzi Alhamisi jioni walikutana na kufanya kikao cha dharura kujadili uamuzi huo wa mwenyekiti wao.
Mtoa taarifa huyo alisema, katika kikao hicho wajumbe hao kwa pamoja walikubaliana kukutana na Manji kumuomba aendelee kuiongoza timu hiyo kwa kipindi chote alichokibakiza.
“Ni ngumu kukubali kirahisi kumuachia Manji aondoke Yanga, kama uongozi tumeipata barua ya Manji ya kuomba kujiuzulu katika nafasi yake, lakini niseme tu huu siyo wakati wake kuondoka.
“Wajumbe tumekataa na tumeikataa barua yake aliyoikabidhi kwa viongozi na jana (juzi) tulikutana na kujadiliana juu ya hilo na tumefikia muafaka wa Manji kuendelea na nafasi yake,” alisema mjumbe huyo.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa kuzungumzia hilo alisema: “Hilo la kikao cha dharura kufanyika kwa wajumbe ni kweli walikutana na kwa upande wangu siwezi kulizungumzia hilo.”
Tupia Comments: