WAKATI baadhi ya watu wa kada mbalimbali, wakiwamo wataalamu wa sheria wakisema mikataba mibovu katika sekta ya madini ni kiini cha serikali kupoteza mabilioni ya fedha kama ilivyoainishwa na Kamati ya Rais, waliopata kuwa wanasheria wakuu wa serikali, Andrew Chenge na Frederick Werema, wamelivua zigo hilo na kuzirushia mamlaka nyingine.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na MTANZANIA Jumamosi, mjini Dodoma na  kwa njia ya simu, wanasheria  hao wametoa kauli zinazofanana, zinazoonyesha kuwa hawahusiki katika uzembe unaosemwa sasa.
Siku tatu zilizopita Kamati ya kuchunguza kiwango cha madini kilicho katika mchanga (makinikia) unaosafirishwa nje ya nchi ilikabidhi ripoti yake, ambayo pamoja na mambo mengine, imeonyesha kuwapo kwa uzembe katika kudhibiti biashara hiyo.
Wakati Chenge na Werema wakiweka msimamo huo sasa, baadhi ya wanasheria, akiwamo Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, mapema wiki hii alindika kuwa; “Tulikosea njia tulipopitisha sheria ya madini ya mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko sheria, tukajifunga pingu. Nani wa kumlaumu?”
Hoja kama hiyo pia imezungumzwa na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Tundu Lissu, ambaye amekuwa akihoji matatizo ya mikataba ya madini, miongoni mwake ikiwamo sheria ya madini ya mwaka 1998, ambayo serikali iliipeleka bungeni kwa hati ya dharura na ikapitishwa ndani ya siku moja.
Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuanzia mwaka 1993 mpaka 2005.
Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa alishuhudia mikataba yote mikubwa ya madini ambayo inalalamikiwa kwa sasa ambayo ilisainiwa kati ya mwaka 1994 mpaka 2007.
Wakati Chenge akiwa AG katika kipindi cha utiaji saini mikataba hiyo, chini ya serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa 1995 – 2005, Jaji Frederick Werema alikuwa mtaalamu wa Sheria katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jaji Werema alishika nafasi hiyo kati ya mwaka 1984 mpaka 2007 na baadaye kuja kuwa Mwanasheria Mkuu kati ya mwaka 2009 hadi 2014, akichukua nafasi ya Johnson Mwanyika, aliyestaafu kwa lazima.

Chenge
Alipotakiwa kuzungumzia kinachosemwa kwamba wakati akiwa AG, Serikali iliingia mikataba mibovu inayoigharimu Serikali kwa sasa, Chenge alisema: “Rais ameshatoa maoni yake, kuna marais mawili hapa? Nani alikwambia nilikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali? Mbona nyie wagonjwa gonjwa kidogo? Mnaonekana kuwa na ugonjwa.
“Unachotaka ni nini? Sina comment nawaambieni. Yawezekana ninyi hamkumbuki historia ya ripoti ya Bomani ambayo ilitoa mapendekezo ili Serikali ione uwezekano wa kufanya smelting (uchenjuaji)  hapa nchini.
“Mtu akikukumbusha kwa jambo jema, atakwambia kwanini hamjafanya tangu kipindi kile, yawezekana mtu anasema requirement ya smelting ni gharama, au production haitoshelezi.
“Lakini, ukikaa kimya italeta maneno, maana madini hayo ni mali ya Watanzania, kwani wengine wanaamini tunaibiwa na wengine hawaamini. Wakizipiga zile hesabu na mimi ukaniambia ni trilioni, nakataa kwa sababu I know it, nadhani kuna mahesabu wameyakosea.”
Chenge alisema suala la madini lina mambo mengi ya kitaalamu na hata kushangaa ni kwanini kila mara amekuwa akinyooshewa kidole.
“Hili suala lina mambo mengi ya kitaalamu. Kwa hiyo, nasema uamuzi wa Serikali kuhusu madini ulikuwa ni huo tu, lakini ukiniambia nilikuwa mwanasheria mkuu, mhhh.
“Chenge anabeba mengi na huwa nawaambia Watanzania kwamba basi Chenge ana akili sana, maana watu wote wananisema mimi. Tulianza mambo ya petroli na Mwalimu, mimi nimesomeshwa mambo ya mikataba ya madini na petroli na watu hawajui, lakini mimi nayajua.
“Utakuta mtu anajidai anajua, mimi namwangalia tu kwa sababu wakati mwingine hajai kwenye kiganja changu. Sijui kuna tatizo gani, Watanzania wananisema mimi nina akili kuliko wote, lakini yote hayo unabeba, mtu mzima unabeba tu, you don’t over react.
“Kwa hiyo, nasema Rais ameamua kuwakumbusheni hayo mapendekezo ya Bomani, kwanini hamkwenda huko ili baadaye muulizane na kuona kama inawezekana au haiwezekani?” alisema  Chenge.
Wakati Chenge akisema hayo, kumbukumbu zinaonesha kuwa, mikataba mikubwa ni Bulyanhulu, ambao ulisainiwa Agosti 5, 1994, Golden Pride ulioko Nzega Juni 25, 1997.
Mingine ni Geita Gold Mine uliopo Geita, ambao ulisainiwa Juni 24, 1999, North Mara uliopo Tarime (Juni 24, 1999), Tulawaka uliopo Biharamulo (Desemba 29, 2003), Buzwagi uliopo Kahama (Februari 17, 2007).
Werema
Kwa upande wake Werema, akizungumza kwa njia ya simu na MTANZANIA Jumamosi, alisema haoni kama kuna tatizo la kisheria katika mikataba ya madini, isipokuwa kuna watu ambao walikuwa hawafanyi kazi yao sawasawa.
Werema, ambaye alionyesha kushangazwa na watu wanaoilalamikia sheria ya madini ya mwaka 1998, baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa ripoti ya makontena yenye mchanga wa dhahabu yanayoonyesha kuwa na kiwango kikubwa cha madini tofauti na kinachotajwa na wawekezaji, aliyafananisha malalamiko hayo na mashtaka ambayo yanataka kudhoofisha hoja ya baadhi ya watumishi kutowajibika sawasawa.
“Suala la sheria mbovu za madini ni general accusation, sheria ya madini ipo na ilikuwa inafanyiwa marekebisho na wakati wangu ilifanyiwa marekebisho mara moja mwaka 2009, sasa anayetuhumu lazima aeleze msingi wa tuhuma zake ni nini? hii  tunayoizungumzia hapa ni practice.
“Nadhani tatizo lililopo ni wataalamu ambao wanalipwa fedha nyingi kwa ajili ya kupima hayo madini yaliyopo katika makontena na walikuwa hawafanyi kazi sawa sawa na tulikuwa tunasema kila siku ni vizuri kila mtu afanye kazi yake kwa ufasaha,” alisema Werema.
Alisema  vipimo vya michanga ya dhahabu vilikuwa vinapimwa na wataalamu na si wanasheria kama wanavyozungumza watu.
“Hili la mchanga ni kilio cha muda mrefu, lakini kwa hali ya kawaida tu lazima jamii ijue, mfano mimi ni mwanasheria, ukiniletea kontena la mchanga wa dhahabu hapo siwezi kujua kilichopo bila kumshirikisha mtaalamu, nadhani hilo ni funzo kwa sababu haya yaliyotokea ni tatizo la wataalamu,” alisema Werema.
Alisema kama vipimo vilivyotumiwa na kamati ni vile vile ambavyo vilikuwa vikitumiwa na wataalamu    katika shughuli zao za kila siku, ni wazi kuna tatizo na wahusika watapaswa wafidie hasara.
Alisisitiza kuwa, sheria ya madini ilitungwa na kundi la wataalamu wa sheria nchini ambao walizunguka katika nchi za Afrika na Uingereza kuangalia sheria zinazohusu mambo hayo zinasemaje, ili  nchi iweze kutengeneza sheria zake.
Alisema kuna haja ya watendaji kuwa makini na waangalifu wanapokuwa wanafanya kazi  na wataalamu kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya Taifa.
MTANZANIA Jumamosi pia limezungumza na mmoja wa maofisa wa ngazi za juu ambaye alipata kufanya kazi katika Wizara ya Nishati na Madini, ambaye hata hivyo ameikosoa Ripoti ya Kamati iliyoundwa na Rais Magufuli.
Ofisa huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa hoja kwamba kazi yake itaharibika, alisema kamati hiyo haikueleza ukweli juu ya usafirishwaji wa madini hayo pamoja na muda uliotumika kuanza kusafirisha mchanga huo kwenda nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji.
“Kama utakumbuka, mwaka 2007, Tume ya Jaji Bomani iliundwa kwa ajili ya kuchunguza mikataba ya madini pamoja na sera ya sekta hiyo. Katika kufanya kazi tume hiyo, iliangalia sera na sheria na mwisho yakawasilishwa mapendekezo yake serikalini kwa utekelezaji.
“Mwaka 2008, mchakato ukaanza wa kubadili sera na mwaka 2009 sera hiyo ikapatikana na mwaka 2010, tukapata sheria mpya.
“Sera hiyo ilisema tuongeze thamani ya madini kwa kujenga smelting area kwa ajili ya kuchenjua mchanga hapa nchini na wakati huo huo, wawekezaji waelimishwe ili wajue namna ya kuomba leseni za uwekezaji huo na namna zitakavyotolewa.
“Kuhusu hoja ya ile kamati, kwamba tumekuwa tukiibiwa madini yetu kwa miaka mingi, kamati hiyo haiko sahihi, kwa sababu migodi inayotoa huo mchanga ni Buzwagi na Bulyanhulu.
 “Mgodi wa Buzwagi walianza kusafirisha mchanga nje ya nchi mwaka 2008 na Bulyanhulu wao walianza mapema mwaka 2002 kama sikosei. Kwa hiyo, wanaposema tumeibiwa kwa miaka 19, sikubaliani nao,” alisema ofisa huyo.
Mwanzoni mwa wiki, moja ya kamati zilizoundwa na Rais Dk. Magufuli, iliwasilisha ripoti yake ya uchunguzi wa mchanga wa madini uliokuwa kwenye makontena yanayosafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji.
Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa mbele ya Rais Dk. Magufuli, kiongozi huyo aliwachukulia hatua baadhi ya watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini walioonekana kushindwa kutimiza wajibu wao na kuisababishia hasara Serikali, kwa kuwa fedha nyingi zilikuwa zikipotea kupitia usafirishaji huo.

Tupia Comments: