JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia walimu wawili na mwanafunzi mmoja kwa tuhuma za kuvujisha mtihani wa Kidato cha Sita unaoendelea Nchini.
Kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kuvujisha mitihani kuwa ni mwalimu Musa Elius (35) na mwalimu Innocent Mrutu (33) mkazi wa Kibamba na mwanafunzi Ritha Mosha.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walinaswa Mei 6, maeneo ya Chang’ombe baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Ofisa wa Baraza la Mitihani la Taifa, Aron Mweteni kuwa Mei 5, katika Shule ya Sekondari Chang’ombe alimkuta Elius akiingia darasani na mwanafunzi Mosha ambaye ni mtahiniwa wa mtihani wa Kidato cha Sita unaoendelea, wakiwa na karatasi yenye maswali na majibu ya somo la Kemia kwa Vitendo.
Alisema baada ya kuwakamata na kuwatilia shaka, ufuatiliaji wa awali ulifanyika kupitia Baraza la Mitihani la Taifa na kubainika kuwa swali hilo ni miongoni mwa maswali ya mitihani ya Kidato cha Sita unaofanyika mwaka huu.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa wote wanaendelea na mahojiano na upelelezi utakapokamilika watachukulia hatua za kisheria.

Tupia Comments: