Mamia ya wakazi wa Kagera waliingiwa na hofu na kukimbia majumba yao Jumapili wakijihami maisha yao kufuatia tetemeko la ardhi lililokuwa limerepotiwa eneo la Muleba, Manispaa ya Bukoba katika wilaya za Misenyi na Karagwe nchini Tanzania.
Mkuu wa Mamlaka ya Jiologia Tanzania (TGD) Abdulkarim Mruma amewataka wakazi wa mikoa minne iliyoko katika Bonde la Ufa wafuatilie habari zinazotolewa na wataalamu wa mamlaka hiyo mara kwa mara.
Ameeleza kuwa mikoa hiyo minne ni Arusha, Kagera, Mbeya na Kigoma ambayo inapitiwa mara nyingi na tetemeko kwa sababu iko katika Bonde la Ufa.
Amesema tetemeko lililopita Jumapili halikuwa na athari kubwa kwa kuwa lilikuwa dogo. Hivi karibuni tetemeko lenye ukubwa wa 5.2 kwa vipimo vya Richter lililorekodiwa eneo la Mahale, Mkoa wa Kigoma bila ya kusababisha maafa makubwa.
Mwaka jana tetemeko lenye ukubwa wa 5.7 kwa vipimo vya Richter lililotokea mwaka jana na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 10 na kujeruhi watu wasiopungua 200 na kuwaacha mamia bila makazi.
Tetemeko la Jumapili ambalo lilidumu kati ya dakika mbili mpaka tatu lilianza saa 01:28am na wakati huo wakazi hao wengi wao walikuwa wameshalala. Baadhi ya wakazi wa kata za Hamugembe, Nyakanyasi na Mafumbo walielezea kuwa wamekesha usiku kucha nje ya nyumba zao, wakihofia huenda tetemeko hilo likatokea tena ambalo lilipiga Manispaa ya Bukoba mwaka jana, na kuua angalau watu 17.
Kwa mujibu wa Mwandishi wa Habari wa Daily News Mkoa wa Kagera, mkazi wa Kata ya Mafumbo Abbas Bin’ omugabi ameeleza hofu ilioenea akisema kuwa wanawake na watoto wanahofia kulala ndani ya majumba yao.
Akizungumza na vyombo vya habari Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu amesema kuwa hapakuwa na mtu yoyote aliyekufa au kujeruhiwa.
“Ninaweza kuthibitisha kuwa mpaka hivi sasa hatujapokea habari zozote kuhusu vifo au majeruhi… watu wanatakiwa kuendelea kuwa na utulivu na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa TGD,” amesema.
Tupia Comments: