Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama ameongoza Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoa hoja ya kufanya mabadiliko ya maamuzi ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambayo ilipendekeza Mbunge Halima Mdee asihudhurie vikao vyote vilivyobaki vya Bunge la Bajeti kutokana na kukutwa na kosa la kudharau mamlaka ya Spika
Waziri Mhagama amependekeza Mhe. Halima Mdee asamehewe kosa alilolifanya ila endapo atatenda kosa lingine la kudharau mamlaka ya Bunge au kuvunja kanuni za Bunge basi utekelezaji wa adhabu uanze mara moja kwa maelekezo ya kiti cha spika tena bila kuitisha kamati yoyote ya Maadili, hoja iliyoungwa mkono na wabunge wengi wa Bunge.
Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya kamati Haki Maadili na Madaraka ya Bunge, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitoa michango yao juu ya adhabu zilizotolewa ambapo kwa nafasi mbalimbali Wabunge kadhaa wakiwemo Mhe. Joseph Selasini, Mhe. Riziki Shangali, Mhe. Kangi Lugola, Mhe. Peter Serukamba, Mhe. Hawa Ghasia, Mhe.Abdallah Bulembo na Mhe. Janeth Mbene walisimama wakiomba Bunge kukubaliana kumsamehe Mbunge wa Kawe Halima Mdee kwani wanaamini amejifunza na kuomba kwake msamaha mbele ya Bunge ilikuwa ni ishara tosha ya kujutia kosa alilofanya.
Kwa niaba ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Almasi Maige ameunga mkono hoja ya Mhe. Halima Mdee Kusamehewa
Tupia Comments: