Kitendo cha Rais wa Marekani Donald Trump cha kuikosoa Korea Kusini hivi karibuni, kutokana na suala zima la mfumo wa teknolojia ya kujihami na masuala ya kibiashara, kunaweza kupelekea kuharibika kwa ushirikiano kati ya Seoul na Washington.
Hali hiyo inatarajiwa kutokea iwapo mgombea urais wa nchi hiyo Moon Jae-in mwenye kuegemea upande wa waliberali atashinda uchaguzi wa urais wiki ijayo nchini Korea Kusini.
Siku ya Jumapili, mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, H.R. McMaster alionekana kupuuzia kauli ya Rais iliyokuwa inaitaka Korea Kusini kulipa Dola bilioni moja kwa ajili ya kituo cha kujihami cha anga za juu (THAAD) chenye uwezo wa kuzuia makombora ambacho kinawekwa katika upande wa mkoa wa kusini mashariki vijijini katika rasi ya Korea.
Kuchangia gharama za ulinzi
McMaster amezungumza Jumapili na Kim Kwan-jin, Mkuu wa ofisi ya Usalama wa Taifa huko Korea Kusini, kuhusiana na pingamizi kali la Serikali ya Seoul katika kubadilishwa kwa makubaliano yaliokuwa yamefikiwa mwaka jana juu ya mfumo wa THAAD.
Katika makubaliano hayo Marekani ilikuwa imekubali kugharimia mfumo huo wa kujihami (THAAD) dhidi ya makombora na kwamba Korea Kusini ilikubali kutoa ardhi, miundo mbinu na gharama za uendeshaji wa kituo hicho.
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na ofisi ya rais wa Korea Kusini, washauri wa usalama wa taifa wa pande zote mbili “walithibitisha” kuwa makubaliano ya mfumo wa THAAD hautabadilika.
Lakini McMaster ameeleza kuwa madai ya Trump ya kutaka ilipe bilioni moja kwa kuwekwa THAAD ni sambamba na matarajio ya umma wa Marekani juu ya suala la washirika wake kuchangia gharama za ulinzi.”
Wakati wa kampeni za urais Marekani, Trump aliikosoa sana Korea Kusini na washirika wengine kwa kulipa sehemu ndogo ya kiwango sahihi ambacho wanatakiwa kuchangia kwa ulinzi wa ziada ambao wanapata kutoka majeshi ya Marekani yaliyoko katika nchi zao.
Hadhi ya mkataba uliopo baina ya Marekani na Korea Kusini (SOFA) ambao umeainisha uchangiaji wa gharama za ulinzi utasainiwa upya ifikapo mwaka 2019.
Chini ya Mkataba (SOFA) wa hivi sasa imeelezwa kuwa Seoul inailipa Washington zaidi ya dola milioni 866 kila mwaka kwa ajili ya vikosi vya jeshi la Marekani 28,000, ikijumuisha gharama za vituo vya kijeshi, na mifumo ya silaha za kisasa zilizowekwa katika Rasi ya Korea.
Hata hivyo Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini Jumatatu amekataa kutoa maoni yake iwapo Seoul iko tayari kuongeza kiwango cha uchangiaji katika ulinzi ili kuweza kukidhi matakwa ya Trump ya dola bilioni moja wakati mkataba mpya wa SOFA utaposainiwa mwakani.
China yapongezwa
Zaidi ya kudai Korea Kusini ilipe bilioni moja kwa ajili ya mfumo wa kujihami wa THAAD, Trump pia amelalamika katika mahojiano wiki iliopita juu ya mkataba wa biashara holela kati ya Marekani na Korea Kusini akiuita ni “mbaya” na amesema “ lazima tufanye mazungumzo tena kuhusu makubaliano hayo au tuusitishe.”
Kitendo cha Trump kukosoa mshirika muhimu wa Marekani katika eneo hilo ni kinyume kabisa cha kauli yake ya kuipongeza China katika hatua yake ya kuiwekea vikwazo zaidi Korea Kaskazini ili kuidhibiti isifanye majaribio zaidi ya nyuklia.
Rais amesema ataizawadia Beijing kwa kuonyesha ushirikiano na kuacha kuiita China kama ni mchakachuaji wa sarafu ya soko la fedha, kama alivyokuwa akisema wakati wa kampeni.
“Fikiria kama nikisema kuwaambia China, “Trump amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la CBS kipindi cha Face The Nation Jumapili, “Haya basi, mbali na hayo, mnaendeleaje na Korea Kaskazini? Pia, tutatangaza kesho kuwa nyinyi ni wachakachuaji wa sarafu ya soko la fedha.”
Katika mahojiano hayo rais amemwita kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuwa “ ni mtu mwerevu sana” kwa vile alivyoweza kujikusanyia nguvu za kidikteta akiwa bado na umri mdogo.
Hali ya Rais wa Marekani ya kubadilisha misimamo, kuwa laini kwa adui na kuweka msimamo mkali kwa mshirika wa karibu na mwenye mafungamano ya muda mrefu katika eneo la rasi ya korea, inaweza kuzidisha chuki kwa wananchi wa Korea Kusini wenye hasira kwa madai yake ya malipo ya mfumo wa THAAD.
Gazeti la Korea Herald, katika ukurasa wa maoni Jumatatu, umesema Trump, “ameweka thamani ya dola ya silaha hiyo mbele kuliko umuhimu wa ushirikiano.”
Gazeti la The Korea Times limechapisha maoni yenye tathmini ifuatayo, “Ni muda mwafaka kwa Korea kuandaa hatua za kukabiliana na sera za Trump ambazo hazitabiriki.

Tupia Comments: