Baraza la usalama la umoja wa mataifa linapanga kufanya mkutano wa siri leo jumanne ilikuchukuwa hatua dhidi ya Korea Kaskazini kutokana na kukaidi agizo lake baada ya nchi hiyo kufanya jaribio la makombora.
Mkutano huo umekuja siku moja baada ya Korea Kaskazini kulalamikiwa kurusha makombora na UN kutishia kuweka vikwazo vipya dhidi yake.
Baraza hilo lilieleza jana kwamba lilikuwa tayari kuchukua hatua dhidi ya Korea kaskazini kwa sababu ya ukaidi wake wa kutofuata amri iliyotolewa mapema ya kusitisha jaribio la nyuklia.
Katika taarifa ya pamoja iliyoungwa mkono na China, baraza hilo lilielezea wasi wasi wa pamoja kuhusu jaribio la jumapili lililoelezewa na Pyongyang kama makombora ya masafa ya kati hadi marefu ambayo yalisafiri kilomita 787 kabla ya kutua ndani ya bahari ya Japan.
Taarifa ya baraza hilo iliita ufyatuaji wa makombora hayo tabia iliyodumaza ambayo inaongeza mivutano katika eneo la Asia mashariki na kwingineko.
Marekani, Japan na Korea Kusini mapema wiki hii wameomba mkutano wa dharura baada ya Pyongyang kurusha kombora Jumapili katika anga za juu zaidi zisizo za kawaida.
Anga hizo ndizo zinazopita silaha za balistika ikiwa ni kiashiria kwamba Korea Kaskazini tayari iko katika uwezo mpya wa teknolojia inayoendeshwa na nguvu ya nishati na mafuta yenye uwezo wa kupaisha kombora hilo mpaka kilometa 4,500.
Mapema Jumatatu, Korea Kaskazini imesema ilifanikiwa kufanya jaribio la kombora jipya la masafa ya kati na marefu, lililosimamiwa na kiongozi Kim Jong Un, lililokuwa linalenga kupima uwezo wake wa kubeba “vichwa vikubwa vya silaha za nyuklia.”
Shirika la Habari la Serikali KCNA wamesema kombora hilo lilirushwa katika pembe ya juu ili isisababishe madhara kwa usalama wa nchi za jirani na kuruka kilometa 787, na kufikia mnyanyuko wa kilometa 2,111.
Japan na Korea Kusini kwa haraka zililaani jaribio jipya la Korea Kaskazini na kuliangalia kama ni tishio kwa eneo na ukiukaji wa azimio la Umoja wa Mataifa.
Jaribio hilo kwa mujibu wa tamko la ikulu ya White House, “inalazimu kuwa ni ilani kwa mataifa yote kutekeleza vikwazo vikali zaidi dhidi ya Korea Kaskazini.”
Tupia Comments: