Taasisi zinazojishughulisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na ukimwi Zanzibar zimetakiwa kuelekeza nguvu katika makundi maalum ambayo maambukizi bado ni makubwa.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alitoa ushauri hao alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa mapambano ya ukimwi uliotayarishwa na Taasisi ya kuimarisha huduma za afya Tanzania (THPS) na kuzindua mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi hiyo katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Alisema wakati Zanzibar inajivunia kuwa na asilimia chini ya moja ya maambukizi ya VVU, katika makundi maalumu maamukizi yapo kwa asilimia 10 hadi 19 ambapo ni hatari.
Aliyataja makundi hayo kuwa ni vijana wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, wanawake wanaofanya biashara ya ngono na wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao.
Alisema kunapokuwa na kikundi kidogo cha watu wenye hali kubwa ya maambukizi ya VVU hatari ya maambukizi inaelekea kwenye jamii.
“Makundi maalum yanaonekana kuwa ni daraja la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwao kuja kwenye jamii, ”alisisitiza Waziri wa Afya.
Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeridhia kuyafanyia kazi malengo ya dunia ya kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU ifikapo mwaka 2030 hivyo mashirikiano zaidi yanahitajika katika kufikia malengo hayo.
Hata hivyo alieleza kuwa ushiriki wa wananchi katika kupima VVU bado hauridhishi na wale wanaopima na kubainika na maambukizi wengi wao hawajiungi kwenye huduma za tiba na wachache wanaotumia dawa hawazitumii ipasavyo.
Waziri wa Afya alikumbusha kuwa wakati huu ambapo Zanzaibar inatekeleza Mpango wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito lakini wanaume hawajitokezi kupima afya zao.
“Akinababa tuwasindikize wake zetu kliniki ili na sisi tupimwe Virusi vya ukimwi, hivi sasa tupo chini ya asilimia tano wakati wenzetu T
anzania Bara wamefikia asilia 80, “Waziri Mahmoud alihimiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa THPS Dkt. Redempta Mbatia alisema katika kupambana na ukimwi Zanzibar, taasisi hiyo imekuwa ikiwajengea uwezo wafanyakazi wa afya na taasisi nyengine zinazoshiriki katika mapambano hayo.
Aidha alisema wamekuwa wakisaidia masuala ya uongozi pamoja kuimarisha utawala bora na kusaidia vifaa tiba katika Hospitali na vituo vya afya ili kuhakikisha huduma za afya zinakuwa endelevu na kufikia malengo yaliyowekwa.
Tupia Comments: