Mwenyekikiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyemaliza muda wake Rais John Magufuli amezitaka Kenya na Rwanda, zinazotarajiwa kufanya uchaguzi mkuu baadae mwaka huu, kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.
Rais Magufuli amesema hayo Ikulu Jijini Dar es salaam wakati wa Mkutano wa Kawaida wa 18 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akisema hatua hiyo itazidisha amani na utawala bora katika nchi za jumuiya hiyo.
Rais Magufuli pia amesema ujenzi wa miundombinu kadhaa ya usafiri inayounganisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki imefikia pazuri.
Amesema katika kipindi cha uenyekiti wake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utekelezaji wa miundombinu hiyo umeenda sambamba na vituo vya usafiri.
Katika mkutano huo Rais John Magufuli amekabidhi uenyekiti kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na pia umemchagua Mhandisi Stephen Daudi Malekela Mlote kutoka Tanzania kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika mkutano huo Uganda imewakilishwa na Rais Yoweri Museveni, Kenya imewakilishwa na Makamu wa Rais William Ruto, Burundi imewakilishwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Gaston Sindimwo, Rwanda imewakilishwa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masuala ya Afrika Mashariki Francois Kanimba huku Sudan Kusini ikiwakilishwa na Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa nchi hiyo Aggrey Tisa Sabuni.
Tupia Comments: