Rais John Magufuli amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa waasisi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (Chadema) Phillemon Ndesamburo huku akimtaja marehemu kuwa alikuwa kiongozi mwenye hekima na aliyezingatia siasa za kistaarabu.
Taarifa iliyotumwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa leo Jumatano imeeleza kuwa Rais Magufuli , ametuma salamu za rambirambi kwa viongozi na wanachama wa Chadema pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo hicho.
“Kwa masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo. Namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake uliozingatia siasa za kistaarabu,”imesema taarifa hiyo
Rais Magufuli amesema alifanya kazi na Ndesamburo wakati wote wakiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakati wote walishirikiana, kutaniana na anamkumbuka kwa namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslahi kwa wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Magufuli ameitaka familia ya Ndesamburo na wote walioguswa na msiba huu kuwa na moyo wa subira na uvumilivu.
Tupia Comments: