Msichana wa miaka 14 aliyejisalimisha alipokuwa akitekeleza shambulio la kujitolea muhanga katika kambi ya jeshi kaskazini mwa jimbo la Maiduguri nchini Nigeria amesema aliteuliwa kutekeleza shambulio hilo kwa kukataa kuolewa na waasi wa Boko Haram.
Amesema alitekwa nyara na babake huko Gwoza, katika jimbo la Borno mwaka 2013, Shirika la habari la Nigeria limesema.
''Nimesalia kwa zaidi ya miaka mitatu katika mikono ya Boko Haram. Wafuasi watatu tofauti wa kundi hilo waliwasilisha ombi la kutaka kunioa lakini nikakataa.
Wawili kati yao walikuwa makamanda.
Nilipokataa kwa mara ya tatu , kamanda mmoja alikasirika na kunitishia kuniua mimi na babangu.
Nilimwambia heri nife kuliko kuolewa na waasi wa Boko Haram.''
''Baada ya wiki moja , wakasema kwa vile nimekataa kuolewa , ninastahili kupelekwa huko Maiduguri kutekeleza mauaji.Watatu wakanishika mikono yangu na wakanidunga sindano.''
Aliambia shirika la habari la Nigeria (NAM) kwamba baadaye alisafirishwa katika kambi ya jeshi pamoja na washambulizi wengine.
Mmoja wao alilipua bomu lake kwenye mkanda wake wa kifuani , lakini lilimua yeye mwenyewe, kwa upande wake mwengine, alisema alipigwa risasi na wanajeshi, Shirika la habari la Nigeria limeripoti.
Alisema hivyo na akatoa mkanda wake wa bomu na kujisalimisha.

Tupia Comments: