Serikali inatarajia kuajiri watumishi 4,339 katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka huo wa fedha.
“Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ujumla wake, inatarajia kuwapandisha vyeo jumla ya watumishi 7,317.
“Kati yao, watumishi 105 ni wa makao makuu ya wizara, askari 5,772 wa Jeshi la Polisi na askari 1,440 wa Idara ya Uhamiaji.
“Katika mwaka huo pia, wizara inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 4,339 ambapo katika makao makuu ya wizara wataajiriwa watumishi 26, Jeshi la Polisi wataajiriwa 2,573, Jeshi la Magereza 500, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 600, Idara ya Uhamiaji 600 na Nida wataajiriwa watumishi 40.
“Pamoja na hayo, wizara itaendelea kuwapandisha vyeo watumishi na askari wake kadiri watakavyopata sifa kulingana na miundo yao ya kiutumishi,” alisema Nchemba.
Wakati huo huo, Nchemba alisema Serikali inatarajia kuanzisha mkoa mpya wa kipolisi Rufiji ili kukabiliana na uhalifu katika maeneo hayo.
“Kutokana na ongezeko la matukio makubwa ya uharifu katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, katika mwaka 2017/18, Serikali inatarajia kuanzisha mkoa mpya wa kipolisi Rufiji.
“Lengo la kufanya hivyo ni kusogeza huduma ya polisi karibu zaidi na wananchi na kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo. Pindi mkoa huo utakapoanzishwa, Wilaya ya Mafia nayo itakuwa ndani ya mkoa huo mpya,” alisema Nchemba.
Akizungumzia uhakiki wa silaha ambazo baadhi zimekuwa zikitumika katika uhalifu, waziri huyo alisema hadi kufikia Machi mwaka huu, asilimia 63.2 ya silaha hizo zilikuwa zimehakikiwa.
“Katika uhakiki huo jumla ya silaha 486 zilisalimishwa kutokana na kutomilikiwa kihalali. Miongoni mwa silaha hizo ni bastola 16, rifle 18, shotgun 161, SMG 24, G3 moja pamoja na magobore 266,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, aliitaka Serikali iimarishe ulinzi katika wilaya za mkuranga, Kibiti na Rufiji ili wananchi wa maeneo hauo waweze kuishi kwa amani.
Tupia Comments: