Jumuiya ya Wanawake wa CUF (Juke- CUF) imewataka wanawake nchini kukataa kushirikishwa au kuwa sehemu ya utekelezaji wa mipango miovu dhidi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Juke-CUF, Fatma Abdulhabib Ferej alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita ikimuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Chama hicho kipo kwenye mgogoro wa uongozi kati ya katibu mkuu huyo na Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Ferej alisema si busara kwa mwanamke kujiingia katika kundi ambalo kwa makusudi linaonekana kwenda kinyume na utaratibu wa sheria uliopo kuhusu vyama vya siasa nchini.
Alisema Juke-CUF ipo tayari kukilinda chama hicho kwa gharama yoyote na kwamba, itasimamia na kutekeleza maagizo yatakayotolewa na CUF.
Ferej alisema mgogoro huo umepandikizwa makusudi ili kufifisha mafanikio ya CUF yaliyopatikana katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Tupia Comments: