SERIKALI kupitia TANESCO imefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya umeme Nchini ambao haujawahi kutokea Katika Historia ya uwekezaji katika Sekta ya Umeme.
Miongoni mwa Miradi mikubwa ya umeme inayotekelezwa ni pamoja na upanuzi wa Kinyerezi I, ujenzi wa Kinyerezi II, Kinyerezi III, Kinyerezi IV, Malagarasi Mkoani Kigoma, Lusumo Falls Mkoani Kagera, Kikonge Mkoani Luvuma, Mkoani Mtwara na mingine mingi.
Kwa upande wa miradi ya ufuaji umeme, Sekta binafsi nayo haikuachwa nyuma katika harakati za ufuaji na usafirishaji umeme Nchini, Kwa kuzingatia kuwa azma ya Serikali ni kufikia ufuaji wa umeme wa Megawati 5,000 ifikapo 2020 na Megawati 10,000 ifikapo 2025. Kwa kuzingatia hilo Serikali ilianzisha mkakati maalum wa kuongeza uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme ambayo inatekelezwa kwa kushirikiana na Sekta binafsi kutoka ndani na nje ya Nchi.
Sekta binafsi imeshirikishwa katika miradi midogo ya Nishati Jadidifu (Renewable Energy) yenye MW 16.29, imetekelezwa na Sekta binafsi, nayo ni Miradi midogo ya kuzalisha umeme wa maji (Min Hydropower) ambayo ni Uwemba- MW 0.84, Mwenga MW 4, na Yori MW 0.95, na Miradi midogo ya kuzalisha umeme kwa kutumia tungamo taka (Biomass) ni Tanwat MW 1.5 na TPC MW 9.0.
Aidha, Katika kuhakikisha kwamba Taifa linapata umeme wa uhakika, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbali mbali za kuongeza na kuimarisha mtandao wa usafirishaji na usambazaji umeme, (National Grid) unaounganisha Nchi nzima kwa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo mengi ya nchi yetu.
Mradi wa kuunganisha Nchi za Tanzania – Uganda (Mwanza – Masaka 220 KV) ambao utaboresha hali ya umeme kwa Kanda ya Ziwa, Ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa Kilovolti 400 kutoka Mkoani Iringa hadi Shinyanga, Mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya umeme ya 400KV kutoka Singida - Arusha – Namanga, mradi huu utawezesha kuboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Mikoa ya Kaskazini.
Miradi mingine ni Mradi wa ujenzi wa njia ya 220 KV (Western spur.) utakaoanzia Tunduma, Sumbawanga, Kigoma mpaka Kyaka, mradi huu utaunganisha katika Gridi ya Taifa, Mikoa ya Songwe, Rukwa, Kigoma mpaka Kagera na hivyo kuboresha hali ya umeme katika kanda ya Magharibi, Mradi wa Chalinze hadi Arusha, Kanda ya Kaskazini (North West Grid), Mradi wa Njombe, Songea na Mbinga (South west Grid), mingine ni ya uzalishaji umeme ya Kinyerezi (Megawati 240), Luhudji (Megawati 400) na mingineyo, Uboreshaji umeme jijini Dar es Salaam, City Centre-Dar es Salaam na Electricity V.
kutokana na uwekezaji huo mkubwa,na uboreshaji wa Miundombinu unaofanywa na TANESCO, hakutakuwa na upungufu wa umeme Nchini, Mwaka 2015 Nchi ilikuwa na upungufu wa umeme wa jumla ya Megawati 300, na maeneo mengine yalikuwa na hali mbaya hususan Mwanza, Arusha na Kilimanjaro lakini kwa sasa hali ya umeme katika Mikoa yote na mingine ni nzuri na hakuna upungufu wa umeme na kama ikitokea umeme umekatika ni matatizo ya kiufundi katika eneo dogo na kwa muda mfupi.
Sambamba na uwekezaji unaoendelea, TANESCO imeongeza juhudi za kusambaza umeme kwa Watanzania wengi zaidi kote Nchini, maeneo ya Mijini na Vijijini. Aidha, katika Takwimu mpya za kiwango cha utumiaji wa umeme Nchini zilizotangazwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ambazo zilizotayarishwa na Wakala wa Taifa wa Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na REA, TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini zinaonesha hadi kufikia Desemba 2016: (i) Watu wenye fursa ya kutumia umeme Nchini (Overall National Access Level) ni 67.5% (2007: ilikuwa 10%) ambapo Vijijini ni 49.5% (2007: ilikuwa 2%) na Mijini ni 97.3%.
Serikali kupitia TANESCO pia inaendelea kuhimiza Wananchi kuunganisha Huduma ya umeme katika maeneo yao ya Vijijini hii ni baada ya utekelezaji wa Miradi Kabambe ya REA kufanikiwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kasi ya Wananchi ya kuunganisha Huduma ya umeme.
Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA TURNKEY PHASE III) ambao umeshaanza kutekelezwa. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 katika Vijiji 7,873 vya Wilaya zote za Tanzania Bara. Takribani Vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa Gridi ya Taifa na Vijiji 176 umeme wa nje ya Gridi (Off-grid).
Mpango huu utaongeza wigo wa usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa na Mradi wa REA II (Turnkey Phase II)
Tupia Comments: