MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa  Tanzania na timu ya KR Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, amesema anaamini timu hiyo itaibuka na ushindi nyumbani katika mchezo wa marudiano  dhidi ya Celta Vigo na kufuzu nusu fainali ya michuano ya Europa.

Genk ilitandikwa mabao 3-2 ugenini na Celte de Vigo ya Hispania katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, hivyo inahitaji ushindi katika mchezo wa marudiano ili kufuzu hatua ya nusu fainali.

Akizungumza jana, Samatta alisema wamefanyia kazi kasoro zilizojitokeza kwenye mchezo wa kwanza na kusababisha wapoteze ikiwemo kupoteza nafasi nyingi za wazi, hivyo wana matumaini ya kupata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano.

Alisema anafahamu mechi ya marudiano itakuwa ya ushindani mkubwa, lakini watalazimika kupambana kufa kupona ili waweze kushinda kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wetu wa marudiano, hivyo tayari benchi la ufundi limeanza kufanyia kazi kasoro  zilizojitokeza kwenye mchezo wa kwanza ili zisijirudie tena,” alisema Samatta.

Samatta kwa siku za karibuni amekuwa tegemeo katika kikosi cha KRC Genk aliyojiunganayo akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya  Kongo (DRC) aliyoichezea kwa mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tupia Comments: