ANACHAMA wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), watakaoacha kazi kabla ya kufikisha umri wa kustaafu, watalipwa mafao ikiwa kuacha kwao kazi kutatokana na sababu zisizozuilika na kuthibitika kutoweza kuendelea kutoa michango, imeelezwa.
Aidha, mfuko huo umesema wanachama wake watakaokimbiwa na waajiri na kushindwa kuendelea kutoa michango kwakuwa ajira zao zimekoma ghafla, watatolewa michango hiyo na Nssf hadi watakapopata ajira au kujiajiri.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana kuhusu kukoma kwa ajira za wanachama na hatma ya mafao yao, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bathow Mmuni, alisema lengo la mfuko huo ni kuwezesha wanachama kujimudu kiuchumi pindi wanapostaafu wakiwa na miaka 55.
Hata hivyo, Mmuni alisema kuna mazingira yanayoangaliwa na vigezo vinavyozingatiwa ili kumlipa mwanachama aliyeacha kazi kwa hiyari. Alisema miongoni mwa vigezo au sababu hizo ni pamoja na mwanachama kuwa na vielelezo vitakavyouthibitishia mfuko kuwa anakwenda kusoma na kwamba hatakuwa mfanyakazi, bali mwanafunzi asiyeweza kuendelea kutoa michango, kuugua au kupata ulemavu unaoonesha wazi kwamba mhusika hawezi tena kujiajiri au kuajiriwa.
“Kuhusu mwanachama aliyeachishwa kazi, NSSF inalitizama suala lake kwa namna tofauti na yule aliyeamua kusitisha ajira yake mwenyewe, kwa sababu azijuazo ambazo sisi kama mfuko hatuzikubali kuwa kigezo cha kumlipa”, alisema.
Zaidi, alisema mfuko huo unamshauri mhusika atafute kazi nyingine, ili aweze kuendelea kutoa michango kila mwezi, hadi atakapofikisha umri wa kustaafu kisheria. Kwa mujibu wa Mmuni, anayeachishwa kazi huwa hapati usumbufu wa kutoa maelezo kama anayeacha kazi mwenyewe, hasa kama anakuwa na viambatanisho muhimu vinavyotakiwa kuthibitisha kuachishwa kwake kazi, kwa sababu mazingira yake yanakuwa yanaeleweka.
Pamoja na hayo, alisema wanachama wasikubali kupotoshwa kwamba msimamo wa Nssf ni kutolipa mafao kwa mwanachama yeyote hata akiwa na sababu hizo zisizozuilika hadi afikishe umri wa kustaafu.
Alisisitiza kuwa ni lazima mfuko huo utekeleze malengo ya kuwa hifadhi ya jamii ili, pamoja na kusaidia wanaostaafu kuwa na fedha za kujikimu, uiunge mkono Serikali kuondoa uwezekano wa waataafu wake kuwa wategemezi.
Aliwataka Watanzania wanaochangia fedha katika mfuko huo kuelewa kuwa Nssf haina fao la kujitoa katika mafao yake saba, bali inaangalia sababu muhimu na kuwalipa wanaojiondoa au kuondolewa kazini.
Kuhusu kulipia waliotorokwa na waajiri, Mmuni alisema inafanya hivyo kupitia akaunti yake ya hasara iitwayo Loss. “Mfano mzuri wa mwajiri aliyewatoroka wafanyakazi ni AMI hospitali, mfuko ulilazimika kubeba jukumu kupitia akaunti hiyo ya hasara hivyo wanachama wasihofu kupoteza haki zao,” alisema.

Tupia Comments: