Mbuge wa Igunga Dk. Dalaly Peter Kafumu amefunguka na kusema kuwa wasaidizi wa Rais wakiwemo wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mawaziri, na wabunge wa upinzani na washauri wa karibu wa Rais wamekuwa wanafiki na kushindwa kumshauri

Dalaly ametoa kauli hiyo kwa madai ya kushindwa kumshauri vizuri Rais Magufuli katika mambo ya msingi ambayo yanaweza kuleta maendeleo katika taifa

Dkt. Kafumu amesema hayo bungeni wakati akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, mbunge huyo anasema viongozi hao wanashindwa kutumia vyema sifa kuu tatu za Rais Magufuli ambazo ndizo zilikuwa zinahitajika kwa muda mrefu.

"Tumepata Rais ambaye sifa zake tatu zilikuwa zinahitajika sana, sifa ya kwanza ana nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa wanyonge, sifa ya pili anaamua papo kwa papo hacheleweshi, sifa ya tatu anataka watu wafanye kazi, sifa hizi sisi baadhi yetu tumezitumia vibaya tumeshindwa kuzitumia vyema ili nchi yetu isonge mbele. Baadhi yetu wabunge wa upinzani na CCM, baadhi yetu mawaziri siyo wote na baadhi yetu wasaidizi wa Rais tumeshindwa kusema kweli, tumeshindwa kushauri kwa ukweli tumekuwa wanafiki na hili jambo litatuua sana" alisema Kafumu

Kafumu anadai wengi wao wamekuwa wakitengeneza ushauri nusu nusu kwa Rais jambo ambalo linafanya zile sifa zake tatu kuu zitumike vibaya, kwa kufanya maamuzi kwenye jambo ambalo huenda halijakamilika.

"Rais anaamua pale pale unafikiri kitatokea nini? tunahitaji uchambue ushauri wako, uupime, uutengeneze ushauri uende umekamilika, na Rais wetu huyu anayefanya papo kwa papo akiamua nchi inasonga mbele, sasa hivi haya yote tunayoyaona ni kwa sababu ya unafiki umezidi miongoni mwetu" alisema Kafumu

Tupia Comments: