Hata wale tunaowaona kama wamekwama kwenye kazi au biashara wanazofanya, wanazo ndoto kubwa.
Mwandishi mmoja aliwahi kusema, sehemu pekee yenye utajiri mkubwa hapa duniani ni makaburini. Siyo kwenye migodi ya dhahabu, wala siyo kwenye viwanda, ila kwenye makaburi.
Maana kule wamelala watu ambao walikuwa na ndoto kubwa sana, lakini hawakuweza kuzitimiza, hivyo wakafa na utajiri mkubwa ndani yao.
Mafanikio ni magumu kwa sababu mbalimbali, zipo sababu za ndani ya mtu mwenyewe, na hapa ndipo unakutana na uvivu, kukosa hamasa, kutokuwa tayari kujitoa, kukosa maarifa sahihi na hata kukosa usimamizi wa karibu wa kuhakikisha unafanikiwa. Hizi ni sababu ambazo mtu akiamua, anaweza kuzivuka yeye mwenyewe. Kama ni uvivu mtu anaweza kuondokana nao kwa kutafuta kile ambacho anapenda zaidi kukifanya, na uvivu unapotea mara moja. Kukosa hamasa pia kunaondolewa na kufanya kile unachopenda. Kama mtu akiiweka vizuri ndoto kubwa ya maisha yake, itampa hamasa ya kuweka juhudi zaidi na hata kwenda hatua ya ziada. Sababu hizi za ndani ni nyingi na ngumu kuvuka, lakini mtu akiamua kweli, anazivuka.
Sababu mbaya zaidi zinazowazuia watu kufanikiwa, ni sababu za nje, na hizi ndiyo zimemaliza watu wengi mno. Nilikuwa sijajua nguvu ya sababu hizi za nje, mpaka pale nilipoanza kufanya utafiti mdogo wa kufuatilia watu kutokana na kile ambacho wanaambiwa na hatua wanazochukua. Nilikuwa naangalia watu wanaosema ndoto zao kubwa mbele ya wengine, wanakatishwa tamaa, kwa kupewa sababu kwa nini hawawezi. Baada ya kuambiwa hayo, wengi wanakubali na kuachana kabisa na ndoto zao.
SOMA; Mambo 7 Yanayokufanya Ushindwe Kutimiza Ndoto Zako.
Sababu za nje ni sababu hatari sana kwa sababu zinatokana na mazingira yetu, na pia zinatoka kwa watu ambao ni wa karibu sana kwetu, watu tunaowaamini na hivyo kuona wanachosema wako sahihi. Wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, ni watu muhimu sana kwetu, ambao wametushauri mengi mpaka tumefika hapa. Hivyo tumekuwa tukiwasikiliza na kuwaamini. Kwa bahati mbaya sana, yapo mengi pia wametushauri ambayo yametuzuia kufikia ndoto zetu.
Hebu niambie kama umewahi kusikia moja ya sentensi za aina hii;
Ni wazo zuri, lakini wewe hutaweza kulifanya....
Wasomi wa aina yako hawawezi kufanya vitu vya aina hiyo....
Watu wa kabila lako hawawezi kufanya hicho unachotaka kufanya...
Acha kupoteza muda wako, hutaweza....
Mbona hapo ulipo ni pazuri, kwa nini usiridhike, unahangaika nini...
Na sentensi nyingine nyingi za aina hiyo.
Najua umeshapata picha na unaziona sura za wale watu waliokuwa wanakuambia hayo maneno.
Na huenda upo hapo ulipo baada ya kufuata ushauri huu wa watu wa karibu kwako. Labda kuna kipaji ulikuwa nacho, na ulitaka kukiendeleza lakini ukaambiwa huwezi kupata fedha kwa kipaji hicho, wewe soma tu uajiriwe. Umesoma na ukaajiriwa lakini unaona maisha kama yamekwama hivi. Au kuna biashara ulikuwa unaipenda na kutaka kuianzisha kwa hatua za chini kabisa, watu wakakuambia acha kujisumbua, huna uwezo wa kuanzisha kwa wakati huo, ukawasikiliza na kuachana nayo.
SOMA; Kama Unataka Mafanikio Makubwa Katika Maisha Yako, Acha Kuogopa Kufanya Mambo Haya.
Sasa leo rafiki yangu, nataka nikupe dawa ya kuweza kuondokana na hiyo hali ya kukatishwa tamaa na watu wa karibu yako. Nataka mazingira yasiwe kabisa sababu ya wewe kushindwa kufikia ndoto zako. Kama utashindwa basi iwe umechagua wewe mwenyewe, na siyo kukatishwa tamaa na wengine.
Ninachokuambia ni hiki rafiki, kataa chochote ambacho hakiendani na ndoto zako. Ndiyo umesoma vizuri kabisa hapo, chochote kile ambacho unakutana nacho au unaambiwa na kinaenda kinyume na ndoto zako, kikatae haraka sana. Usikubaliane nacho hata kidogo. Yaani kwa kifupi, kifute kabisa, wala kisiendelee kukusumbua.
Kwa mfano kama ndoto yako ni kuwa mfanyabiashara mkubwa au mwekezaji mkubwa, unachohitaji kufanya sasa ni kuanza kidogo. Sasa kama akitokea yeyote akajua ndoto yako na kukuambia haiwezekani na kuja na sababu zake nyingi kwa nini huwezi, mwambie HAPANA, halafu achana naye. Wala usitake kubishana naye, usijaribu kumshawishi kwa nini unaweza, wewe mwambie MIMI NITAFIKIA NDOTO HII NA SIHITAJI WA KUNIAMBIA KWA NINI SIWEZI, AFADHALI ANAYENISHAURI NIFANYEJE ILI NIWEZE.
SOMA; Hiki Ndicho Kitu Kikubwa Kinachozuia Kwenye Mafanikio!
Unahitaji kabisa uwe mkali kiasi hichi, watu wajue kabisa wakija kwako hawajiongeleshi tu wanavyojisikia wenyewe, wajue kama ni maoni wanayo basi ni maoni ya kujenga na siyo maoni ya kukatisha tamaa. Usipokuwa makini na mkali juu ya ndoto yako kubwa, utaishia kuwa na maisha ya kawaida kama wengi ambao wameangushwa na maneno ya wengine.
Narudia tena rafiki, chochote ambacho hakiendani na ndoto zako kubwa kikatae, hata kama ni tafiti za kitaalamu, ambazo zinasema watu wenye sifa kama zako hawawezi kufanikiwa, usizisome, maana zitaanza kukudanganya. Wewe tafuta vile ambavyo vinaendana na kile unachotaka, utajifunza mengi zaidi na hata kama utashindwa, basi angalau utakuwa umeshindwa kwa kujaribu, kuliko kushindwa ukiwa umekaa tu.
Ndoto kubwa ya maisha yako inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kwako, usiruhusu wengine waichezee kama wanavyotaka wao, iheshimu na wengine nao wataiheshimu. Uzuri ni kwamba wengi wakishajua msimamo wako juu ya ndoto yako, wanajikuta wakikusaidia kuifikia, wakishajua wewe hutetereki kwenye kile unachotaka, wanakuwa wa kwanza kukupa njia na mbinu nzuri za kufika kule unakotaka kufika.
Tupia Comments: