MKAZI wa kijiji cha Tingeni wilayani hapa Mkoani Tanga, Philipo Fred Elias (45) ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana kwa kutumia panga wakati akirejea nyumbani kwake akitokea kijiji cha Kerenge kwenye shughuli zake.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedckt Wakulyamba, alisema kuwa mtu huyo alifikwa na mauti hayo juzi wakati akirejea nyumbani kwake katika kijiji cha Kerenge saa 2:00 usiku akitokea kijiji cha Tingeni.

Alisema mtu huyo akiwa njia kurejea kijijini kwake akiwa na pikipiki ghafla alikutana na watu ambao idadi yao haijulikani walimsimaisha na kuamkamata na kuanza kumchinja kwa kutumia panga hadi kufariki.

Kamanda Wakulyamba alisema mauaji hayo yalifanyika katikati ya pori linalounganisha kijiji cha Tingeni na Kerenge ambapo vijana waliofanya tukio hilo walikimbia kusikojulikana.

Aliongeza kuwa mwili wa marehemu uligundulika na wapiti njia ukiwa pembeni mwa barabara na pikipiki yake ikiwa imetelekezwa ndipo zilifanyika jitihada za kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji ambao nao waliwataarifu polisi.

Hata hivyo, alisema kuwa marehemu alikuwa akituhumiwa kwa vitendo vya ujambazi na unyang’anyi wa kutumia nguvu na tayari enzi ya uhai wake ameshakamatwa mara kadhaa kwa matukio hayo na kufikishwa katika kituo cha polisi kwa tuhuma za ujambazi.

Kufuatia tukio hilo, jeshi la Polisi linafanya msako wa kuwasaka na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo ya kinyama ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule Wilaya ya Muheza.

Kamanda Wakulyamba ametoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kubwa la jinai kama mtu wanamtuhumu anavitendo vya ujambazi wamkamate wampeleke polisi.

Tupia Comments: