KAMATI ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani ipo katika hatua za mwisho kutatua kero tatu zilizobaki kati ya 15 zilizokuwa zinaukabili Muungano.
Ufumbuzi wa kero hizo 12 ni sawa na kufikia umalizaji wa matatizo ya Muungano kwa asilimia 80, hatua ambayo ni ya kujivunia hatua iliyofikiwa na chombo hicho. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati akizungumza mjini Dodoma jana na waandishi kuhusu mafanikio ya Muungano wa Tanzania ambao wiki ijayo unatimiza miaka 53.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika Aprili 26, 1964 . Makamba alisema, sherehe hizo za Muungano ambazo mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli zitaonesha kwa namna gani muungano unaendelea kuimarika. Makamba alisema kero ambazo bado zinazungumwa ni vyombo vya moto vya usafiri kutoa huduma ya usafiri au kutumika katika pande zote mbili.
“Hiyo ilihitaji kutungwa kwa sheria mpya ya usafiri barabarani, hivi sasa mchakato wa kutunga sheria unaendelea na tayari waraka upo umeshaandaliwa,” alisema. Makamba alisema kero nyingine ambayo mazungumzo yanaendelea ni ya hisa za Zanzibar za iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, ambayo Zanzibar alikuwa mjumbe wake na mara ilipokufa, hisa zake zilihamishiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na akasema nyaraka zipo zinazoonesha suala hilo.
Kero ya tatu, ni kuanzishwa kwa akaunti ya pamoja ili kuangalia fedha za mapato zinazoingia kupitia Benki Kuu ya Tanzania ambazo haziingii kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar. Alisema mazungunzo yanafanyika ili kuwapo mgawo wa mapato ya fedha za akaunti hiyo na namna gani itafanyika kuhusu kuchangia Muungano na ripoti yake itatolewa wakati wowote mwaka huu.
Makamba alisema katika kipindi hiki chote pamoja na changamoto hizo, Muungano umepata mafanikio makubwa yakiwamo ya kuongezeka kwa mambo ya Muungano kutoka 11 hadi 22, na hata kuimarika kwa uhusiano katika mambo ambayo si ya Muungano yakiwamo ya afya, elimu na kilimo. Makamba alisema Muungano huo umeimarisha udugu uliokuwapo kwa miaka mingi, viongozi walikuja kurasimisha na umefanikiwa kutokana na waasisi kukubaliana kwa hiari.
Akizunguzia maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi, wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema yatapambwa na gwaride, maonesho ya makomandoo, mbwa na farasi, kikundi cha wanafunzi wa Dodoma na burudani zikiwamo bendi mbalimbali.
Mhagama alisema, sherehe hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa na serikali, wastaafu, mabalozi, wabunge na wajumbe wa baraza la wawakilishi, wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi.
Mgeni rasmi, ambaye ni Amri Jeshi Mkuu, Rais Magufuli, atapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake na atashuhudia maonesho mbalimbali pamoja na buruduni zitakazokuwa zinafanyika uwanjani hapo.
Aliwakaribisha wananchi wote kufika kushuhudia sherehe hizo za kwanza za kitaifa kufanyika mjini Dodoma tangu serikali imehamia, wananchi ambao watakosa nafasi ya kuingia ndani ya uwanja wa Jamhuri wenye uwezo wa kuchukua watu 17,000, wataangalia maadhimisho hayo moja kwa moja kwa kuangalia kwenye skrini za televisheni ambapo zitakuwa zimefungwa nje ya uwanja.
Mhagama alisema, maadhimisho yatakayokuwa yakiendelea ndani ya Uwanja wa Jamhuri pia yatakuwa yakirushwa moja kwa moja kwenye vituo vya televisheni za TBC, Star TV, Azam na ITV

Tupia Comments: