Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump amesherehekea jana Jumamosi(29.04.2017), siku 100 akiwa madarakani katika Ikulu ya White House pamoja na kundi la watu wakimshangiria katika mkusanyiko unaofanana na mkutano wa kampeni.
akisifia mafanikio yake ya mwanzo na kuwashambulia wakosoaji ambao wametoa alama mbaya kwa utawaal wake.
Trump aliliambia kundi la watu waliokusanyika kwamba ndio kwanza anaanza kutimiza ahadi zake za wakati wa kampeni. Ameshambulia mara kwa mara vyombo vya habari alivyosema ,"havina uwezo, visivyokuwa wa kweli" , akisema havikuwa vinasema ukweli juu ya mafanikio ya utawala wake.
"Utawala wangu umekuwa ukileta mafanikio kila siku kwa wananchi wa nchi hii," Trump alisema mjini Harrisburg, Pennsylvania. "Tunatimiza ahadi zetu moja baada ya nyingine, na kwa hakika watu wanafurahi sana juu ya hilo."
Mkutano huo ulifanyika katika siku hiyo hiyo ambapo maandamano ya mabadiliko ya tabia nchi yalipofanyika ambapo maelfu ya waandamanaji waliizunguka Ikulu ya White House , na pia imeingiliana na hafla ya chakula cha usiku kwa ajili ya waandishi habari kila mwaka maarufu kama tai nyeusi katika Ikulu ya White House mjini Washington.
Trump na wafanyakazi wake waliamua kutohudhuria chakula hicho cha usiku na waandishi habari kwasababu ya kile alichosema vyombo vya habari kutomtendea haki. Trump amesema amejisikia vizuri kuwa mbali na kile alichokiita "kundi la Washington", akiwa na maana waandishi habari.
"kundi kubwa la wacheza sinema wa Hollywood pamoja na vyombo vya habari mjini Washington wanajipongeza katika hafla iliyotayarishwa katika hoteli katika mji wetu mkuu ," Trump alisema huku kundi hilo la watu wakizomea. "Iwapo kazi ya vyombo vya habari ni kuwa waadilifu na kusema ukweli, vyombo vya habari vinastahili kipimo kikubwa kabisa cha kushindwa.
Mafanikio ya Trump
Trump aliorodhesha kile alichosema ni baadhi ya mafanikio yake muhimu , ikiwa ni pamoja na mafanikio ya kuthibitishwa kwa jaji wa mahakama kuu Neil Gorsuch na kusafisha njia kwa ajili ya sheria nyingine nyingi kuhusu mazingira na biashara.
Pia ameorodhesha idhinisho lake kwa bomba la mafuta la Keystone XL na Dakota, akiuwa makubaliano ambayo bado hajaanza ya kibiashara na mataifa ya Asia, na kuimarisha hatua za kiusalama ambazo zimesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa watu kuvuka mipakani kimagendo katika mpaka wa kusini.
"Dunia inapata ujumbe: Iwapo unajaribu kuingia nchini Marekani kinyume na sheria , utakamatwa, kufungwa, kurejeshwa nyumbani kwenu ama kufungwa gerezani," Trump alisema.
Amepuuzia kushindwa kwake kupata ushindi muhimu katika ahadi yake ya msingi wakati wa kampeni, kama kuondoa na kuweka mpango mbadala wa sheria ya matibabu nafuu pamoja na ujenzi wa ukuta katika mpaka na Mexico. Marufuku kwa wasafiri wanaotembelea nchini Marekani kutoka mataifa ya Kiislamu aliyojaribu kuweka Trump , ilizuiwa mahakamani.
Amewalaumu Wademokrats kwa kushindwa sheria hiyo hadi sasa na kusema ahadi zake zote zitatimizwa hatimaye.
"Tutajenga ukuta jamani, wala msiwe na wasi wasi juu ya hilo," amesema.
Baadhi ya waungaji wake mkono katika kundi hilo la watu wamesema wako tayari kumpa Trump muda zaidi.
"Nilimpigia kura na nitampa mwaka mmoja. Inatosha kuliweka baraza la Congress katika hali bora na kuwezesha baadhi ya mambo kufanyika," amesema Michael Casciaro , mwenye umri wa miaka 54, mkandarasi raia katika jeshi.
Tupia Comments: