Klabu za jiji la Manchester, City na United, zitakabiliana leo katika mechi ya Ligi Kuu ya England, ushindani ukizidi kushika moto miongoni mwa timu zinazopigania kumaliza katika nne bora.
David Silva kuna shaka huenda asiweze kuchezea Manchester City baada ya kuchechemea na kuondoka uwanjani klabu hiyo ilipolazwa na Arsenal 2-1 katika nusufainali Kombe la FA.
Sergio Aguero, aliumia kwenye mechi hiyo lakini yuko sawa kucheza.
Gabriel Jesus pia yuko sawa kucheza baada ya kuumia mguuni, lakini meneja Pep Guardiola amesema hali yake si "nzuri kabisa".
Manchester United watakuwa bila Paul Pogba anayetatizwa na misuli, lakini Ander Herrera anaweza kuwachezea.
Chris Smalling na Phil Jones pia wanauguza majeraha, sawa na mshambuliaji Zalatan Ibrahimovic.
Guardiola amesema: "[Jose Mourinho nami] ni majirani. Tunapokutana huwa twasalimiana.
"Wao [Manchester United] ni wazuri. Wapinzani wazuri, wanaocheza vyema na ambao wamecheza kwa muda Ligi ya Premia bila kushindwa..."
Na kuhusu hali kwamba Guardiola hajashinda kikombe msimu huu amesema: "Nimekuwa mkufunzi kwa miaka tisa lakini huu ni wangu wa kwanza bila kombe. Lazima siku moja ingetokea. Itatokea tena iwapo nitaendelea kwua mkufunzi."
Upande wake Jose Mourinho amesema: "Hii inahusu klabu, timu, na nafasi mwisho wa msimu. Si kuhusu mimi na Guardiola.
"Nahisi msimu huu ni muhimu sana kwangu na wachezaji na klabu.
"Unaweza kuwa msimu wa kwanza wa misimu mitano au sita au saba ijayo, lakini unaweza kuwa msimu wa kwanza wa miaka ya ufanisi."
Marcus Rashford alifunga bao Manchester United walipolaza City 1-0 uwanjani Etihad.
Hii itakuwa debi ya kwanza ya Manchester kucheza Alhamisi tangu Novemba 1994 pale mabao matatu ya Andrei Kanchelskis yalipowapa United ushindi wa 5-0 Ligi ya Premia.
City wameshinda mechi tano kati ya nane za karibuni zaidi ligini, na mechi moja kati ya mbili walizoshindwa ilikuwa msimu uliopita kutokana na bao la Marcus Rashford.
Jose Mourinho amemshinda Pep Guardiola mechi moja pekee katika mechi tano za ligi.
Real Madrid chini ya Mourinho walishinda 2-1 dhidi ya Barcelona chini ya Guardiola Aprili 2012.
Tupia Comments: