Hydom mbioni kuwa Mamlaka ya mji mdogo



MAPENDEKEZO ya kuwa na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hydom mkoani Manyara yamejadiliwa katika vikao vya awali vya Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, Bunge limeezwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alitoa taarifa hiyo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay (CCM) aliyetaka kujua ni lini serikali itaupa mji wa Hydom hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo.
Naibu Waziri Jafo alisema mapendekezo hayo yalijadiliwa katika vikao vya awali vya kamati vilivyofanyika Septemba 25, 2012, Baraza la Madiwani katika kikao cha Oktoba 19, 2012 na Kamati ya Huduma za Uchumi katika kikao cha Juni 13, 2014.
Alisema kimsingi vikao vyote vimekubaliana na wazo la kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Hydom.
“Tunashauri mapendekezo hayo sasa yawasilishwe katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) ili hatimaye yawasilishwe kwa waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kupata kibali. Hivyo taratibu hizo zikikamilika na kuonekana mamlaka hiyo imekidhi vigezo, Ofisi ya Rais – Tamisemi, haitasita kuanzisha hiyo kisheria,” alisema Jafo.

Tupia Comments: