MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema kuanzia sasa atapendekeza kwa Rais John Magufuli kutumbuliwa kwenye nafasi zao mara moja watendaji wakuu wa serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma, ambao watashindwa kutekeleza mapendekezo yake kuhusu usimamizi na uendeshaji wa ofisi zao.
Kauli hiyo ya Profresa Assad imekuja wakati ambapo katika ripoti yake ya ukaguzi, iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli na baadaye bungeni hivi karibuni ikiishia Juni 30, 2016, inaonesha kuwa mapendekezo 100 kati ya 234 yaliyotakiwa kufanyiwa kazi katika maeneo mbalimbali hayajaguswa kabisa. Mapendekezo hayo ni yale yalitolewa katika ukaguzi wa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2015.
Akizungumzia hatua hiyo katika mahojiano maalum na Habari- Leo, CAG Assad alisema; “Hatuna cha kufanya kwa watendaji wakuu wa idara za serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma zaidi ya kushauri kwa mamlaka yao ya uteuzi ambayo ni Rais kuwaondoka maana ni sawa na kusema wameshindwa kazi”.
Aidha akijibu swali kama kutofanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa cha mapendekezo katika ripoti yake ya hivi karibuni, kunaweza kufanya ofisi ya CAG kupoteza umaarufu ilioupata katika miaka ya hivi karibuni, ambapo ripoti yake ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na wananchi; Profesa Assad alisema; “Sidhani kama hilo linaweza kushusha umaarufu wetu”.
“Kimsingi kazi yetu sisi ni kukagua na kutoa mapendekezo kwa kile tunachokiona na baada ya hapo Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wanawajibika kuisimamia serikali katika utekelezaji wa mapendekezo yetu, kwa hiyo mwisho wa siku serikali ndiyo inayowajibika kuhakikisha mapendekezo yetu yanafanyiwa kazi na maofisa wake.
“Kwa sasa tutakachokifanya kwa watendaji wakuu ambao watashindwa kutekeleza mapendekezo yetu pale tutakapokagua tena katika mwaka mwingine na kuona upungufu ule ule itakuwa ni kumshauri mamlaka yao ya uteuzi ambaye ni Rais kuwaondoa katika nafasi zao haraka,” alisema Profesa Assad. Hivi karibuni Profesa Assad aliibua ubadhirifu mkubwa wa fedha na mali uliofanyika katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma.
Mbali ya kuwepo kwa ubadhirifu, lakini pia CAG katika ripoti yake ya mwaka wa fedha wa 2015/2016, aliibua dosari za usimamizi au uendeshaji mbaya wa ofisi na mashirika ya umma, hatua iliyoathiri ufanisi au kupunguza tija.
Kwa upande wa mashirika ya umma, ubadhirifu uliibuliwa katika Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Benki ya Twiga, Benki ya Wanawake, ubia baina ya Shirika la Taifa la Madini (Stamico) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Dosari kwa kundi hilo, ambazo zimeathiri uendeshaji wa mashirika ya umma zilibainika katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na makampuni ya madini.
Kwa upande wa serikali kuu na serikali za mitaa, ubadhirifu mkubwa uliibuliwa katika maeneo ya misahamaha ya kodi, ulipaji wa mishahara hewa, usimamizi na matumizi ya fedha za serikali, usimamizi wa miradi, manunuzi ya umma na ubovu wa mikataba.
Dosari ambazo hazina uhusiano na ubadhirifu, lakini ambazo zimeathiri tija katika uendeshaji wa serikali kuu na serikali za mitaa ni katika uandaaji na utekelezaji wa bajeti, usimamizi wa deni la taifa, ucheleweshaji wa michango kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na malimbikizo ya madai ya wafanyakazi.
Pia zipo dosari za usimamizi wa mali na madeni ya serikali, uwepo wa mali za kudumu za serikali zilizotelekezwa, ukarabati wa majengo ya serikali na uendelezaji wa viwanja vya serikali katika balozi za Tanzania nje ya nchi na usimamizi wa rasilimali watu hasa kutokana na watumishi wengi wa umma kukaimu nafasi walizonazo kwa muda mrefu kinyume cha sheria.

Tupia Comments: