Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Benson Bana amesema kuwa kitendo kilichofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kimewafungua macho viongozi wengi wa Afrika na dunia na kitakuwa ni mfano wa kuigwa kwa Serikali nyingi za Afrika na dunia kwa ujumla.

Dkt. Benson Bana amesema hayo wakati akiongea na Idara ya Habari (Maelezo), ambapo ameeleza kuwa kitendo cha kutafuta ukweli katika makinikia na biashara ya madini na kuweka wazi taarifa hiyo kwa umma na kusema wahusika wa sakata hilo wachukuliwe hatua za kisheria kimeonyesha uzalendo wa dhati kwa nchi yake.

“Ningefurahi kama tungetenga siku maalumu kuandamana kwa nia ya kuunga mkono nia njema ya Rais ya kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi hii hazitumiwi hovyo hovyo” amesema Dk Bana.

Pia, Dkt. Benson Bana ameunga mkono kitendo cha Rais kukubali kufanyia kazi mapendekezo yote 21 yaliyotolewa na Tume ya Uchunguzi, kwani yataweka wazi mwenendo mzima wa biashara ya madini na kuziba mianya ya wizi wa madini.

Aidha, Amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kwa kuchukua uamuzi wa haraka wa kuwazuia kusafiri nje ya nchi watuhumiwa wa sakata hilo.

Dkt. Benson Bana ameongeza kuwa wale wote waliotajwa kuhusika na suala hilo kukaa nje ya utumishi wa umma kwa muda wakati uchunguzi dhidi yao ukiendelea na endapo watabainika kuwa hawana hatia warudishwe kazini na ikibainika kuwa walihusika wachukuliwe hatua stahiki, huku akitoa wito kwa Watanzania kuuunga mkono  nia njema ya Rais Magufuli kwa sababu hatua hiyo ni harakati za kuweka sawa uchumi wa nchi ili kuboresha maisha ya Watanzania.

Kufuatia uamuzi huo wa Rais Magufuli kuhusu Makinikia, baadhi ya wasomi wameonyesha kuridhishwa na kuunga mkono hatua ya Rais kuagiza wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria baada ya kupokea ripoti ya pili ya Kamati ya Wachumi na Wanasheria aliyoiunda kwa ajili ya kuchunguza Mchanga wa Madini unaosafirishwa kwenda nje ya nchi.

Tupia Comments: