Mzozo mwingine mpya umekikumba chama tawala nchini Afrika Kusini ANC, wakati rais Jacob Zuma anapokabiliwa na shutuma nyingine mpya za kufichuliwa kwa barua pepe zinazodai mahusiano ya muda mrefu ya Gupta na serikali
Barua pepe hizo zilizotajwa  na magazeti yanayoongoza nchini humo ambayo hutoka mwishoni mwa wiki la Sunday Times na The City Press, zilikuwa na mawasiliano yanayofichua namna ambavyo familia hiyo ya Gupta kwa kiasi kikubwa ilivyoweza kulidhibiti baraza la mawaziri, taasisi za serikali, sera za serikali pamoja na maamuzi yake.
Barua pepe moja inafichua kwamba familia ya Gupta ilipewa wasifu wa waziri wa nishati Mosebenzi Zwane, mwezi mmoja kabla ya kuteuliwa na Rais Zuma. Barua pepe nyingine inaonyesha waziri Des van Rooyen aliyeteuliwa na Zuma kuchukua nafasi ya waziri wa fedha Nhlanhla Nene na kumuondoa baada ya siku nne wakati uchumi wa nchi hiyo ukiwa katika mtikisiko mkubwa, na yeye alisafiri kwenda dubai, safari ambayo inaelezwa iligharamiiwa na familia hiyo ya Gupta.
Barua pepe nyingine inaonyesha mawasiliano kati ya aliyekuwa waziri wa mawasiliano Faith Mutambi na Gupta, wakijadili kuhusu mikakati ya sera za serikali. Katika moja ya barua pepe hizo, kuna nakala ya barua kutoka kwa Zuma kwa mamlaka katika Falme za Kiarabu. Nakala hiyo inaonyesha Zuma akidai kwamba amechagua eneo hilo kuwa makazi yake ya pili.
Hili limewaghadhabisha wapinzani, ambao hivi sasa wanalitaka bunge kuanzisha mchakato wa uchunguzi kamili kuhusiana na mienendo ya Zuma. Kiongozi wa Chama cha Democratic Alliance Mmusi Maimane ameliambia shirika la habari la DW kwamba chama chake kinaandaa utaratibu wa kumfungulia mashitaka Rais Zuma
Südafrikaner fordern Präsident Zuma zum Rücktritt auf (Reuters/S. Sibeko)
Miito imezidi kutolewa nchini Afrika Kusini ya kumtaka Zuma kuachia madaraka
.
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa Afrika Kusini Sithembile Mbete, ameiambia DW kwamba madai hayo yana uzito mkubwa kwa rais, lakini akionya kwamba Zuma anaweza kuruka kihunzi hicho, baada kushinda mara mbili kwenye madai mazito dhidi yake huko nyuma. 
Katika hatua nyingine, mwanasheria wa familia ya Gupta Gert Van der Merwe amepinga taarifa hizo za barua pepe, akidai kwamba kwanza angetaka kuhakikisha ukweli wake. 
Kufichuliwa huko kunakuja muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa juu wa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha ANC, ambapo katika mkutano huo Zuma aliepuka kura ya kutokuwa na imani naye kutoka kwa wanachama wa chama chake. Katibu mkuu wa ANC Gwede Mantashe aliwaambia wanahabari mjini Johannesburg kwamba kuna majadiliano mazito kuhusiana na suala hilo, huku wengine wakiunga mkono wengine wakipinga, na wengine wakiwa katikati. Hata hivyo hakukuwa na hatua zilizochukuliwa.
Mantashe amesema kuongezeka kwa miito ya kumtaka Rais Zuma kuondoka madarakani kunawanufaisha zaidi wapinzani katika hatua zao za kuking'oa chama hicho kilichoongoza nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa makaburu mwaka 1994.
Wengi ndani ya chama hicho bado wanazungumzia matokeo mabaya ya chama hicho cha ANC katika chaguzi za ndani mwaka jana, kutokana na kashfa zinazomkabili rais. Lakini pia wamezungumzia kuporomoka kwa ushawishi wake wakati nchi hiyo wakati ikielekea kwenye uchaguzi mwaka 2019.

Tupia Comments: