KIKOSI cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga kimerejea jijini Dar es Salaam jana na kusema kuwa mechi yao ya kesho dhidi ya Prisons itakuwa ngumu na yenye changamoto lakini wamejiandaa vyema kuwakabili 'Maafande' hao kutoka Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa kucheza na timu moja ambayo uliifunga ndani ya muda mfupi inahitaji nguvu na mbinu za ziada ili kupata ushindi.

Meneja huyo aliongeza kuwa hawawahofii Prisons lakini wanajipanga kupambana ili kusaka ushindi katika mchezo huo na kuendeleza mbio za kutetea ubingwa wanaoushikilia.

"Itakuwa mechi ngumu kwa sababu tumewafunga hivi karibuni, tunaijua Prisons kuwa moja ya timu zenye wachezaji wanaofanya mazoezi kwa muda mrefu, lakini silaha yetu ni moja, kila mechi kwetu tunaingia uwanjani tukiona ni sawa na fainali," alisema Meneja huyo.

Aliongeza kuwa kila mchezaji anafahamu nafasi ya Yanga kushiriki katika mashindano ya kimataifa mwakani imebakia kwenye mechi za ligi hivyo ushindi pekee ndiyo utafanikisha kutimiza ndoto zao baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la FA na Mbao FC ya jijini Mwanza.

Baada ya mechi hiyo ya kesho, Yanga watazialika kwenye Uwanja wa Taifa Kagera Sugar, Mbeya City, Toto Africans na watamaliza msimu huu ugenini kwa kuwafuata Mbao.

Tupia Comments: