Meneja wa Arsena, Arsene Wenger, amesema hatima yake katika klabu hiyo itaamuliwa katika mkutano wa bodi ya klabu hiyo baada ya fainali ya Kombe la FA mnamo 27 Mei.
Mfaransa huyo wa miaka 67 amekuwa na Gunners tangu 1996 na mkataba wake wa sasa unafikia kikomo mwisho wa msimu huu.
Arsene Wenger alianza kazi Arsenal 1996 baada ya kuwa na Nagoya Grampus Eight nchini Japan
Wenger amekuwa akishutumiwa sana na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo, na kunao ambao wamekuwa wakiweka mabango kumtaka ajiuzulu.
“Kuna mambo mengi ambayo yatajadiliwa katika mkutano wa bodi. Moja, ni nini hatima ya meneja,” amesema.
“Bila shaka nitakuwepo. Kwa sasa tunafaa kuangazia yaliyopo sasa na ni kwamba tunacheza Jumapili na tuna fainali ya Kombe la FA.”
Klabu hiyo ya London kaskazini itakutana na mabingwa wa ligi Chelsea uwanjani Wembley, ikiwa ni tumaini pekee la Arsenal kushinda kikombe msimu huu.
Metal magnate Alisher Usmanov anamiliki share kubwa katika klabu ya Arsenal 30.04%
Arsenal wamesalia kucheza mechi moja pekee ligini, ambapo wana kibarua cha kujaribu kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwani wamo nafasi ya tano, alama moja nyuma ya Liverpool walio nafasi ya nne na tatu nyuma ya Manchester City, lakini wanapungukiwa na mabao.
Arsenal watakuwa wenyeji wa Everton mechi ya mwisho Jumapili (15:00 GMT), nao Liverpool watakuwa wenyeji wa Middlesbrough uwanjani Anfield nao Manchester City wasafiri Watford.
Wenger aliongeza: “Lazima tufanye kazi yetu, sisi ni wataalamu na tunataka kushinda. Tumekuwa katika mbio nzuri na tunachoweza kufanya kwa sasa ni kushinda mechi yetu ya Jumapili. Baada ya hapo, kitakachotendeka kunihusu si muhimu.”
“Niko hapa kuitumikia klabu na njia bora zaidi ya kufanya hivyo ni kushinda mechi ijayo.”
Tupia Comments: