Sakata la Serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni limeibuka upya, safari hii ukielekezwa kwa Rais John Magufuli.
Hata hivyo, shughuli nyingi zinazomshirikisha Rais zimekuwa zikirushwa moja kwa moja jambo lililomfanya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Aida Khenani kuhoji sababu za kuzuia shughuli za Bunge kuonekana moja kwa moja.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Khenani alisema Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatumia kodi za wananchi lakini vikao vya wabunge waliowachagua havionyeshwi moja kwa moja kuwawezesha kufuatilia wanachozungumza wawakilishi wao.
“Hapo kuna tatizo,” alisema Khemani.
Alihoji kama tatizo ni gharama kama Serikali ilivyoeleza, inakuwaje pale Rais anapozungumza gharama zinapungua na Bunge linaporushwa moja kwa moja ndiyo zinakuwa kubwa.
Khenani aliungwa mkono na mbunge mwenzake wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha aliyehoji sababu za Bunge kuwa na hofu ya vikao vyake kuonekana moja kwa moja.
Wabunge hao waliungana na mtangazaji wa zamani wa shirika hilo, Juma Nkamia (Chemba-CCM) aliyesema mwishoni mwa wiki kuwa shirika hilo limefika mahali pabaya hadi kuazima mitambo kwa watu binafsi kwa ajili ya kurusha matangazo ya ziara ya Rais Magufuli mkoani Mtwara.
Nkamia amesema hata studio inayotumika TBC ni ile iliyokuwapo tangu enzi za TVT na kwamba shirika hilo lina usikivu mbovu wa matangazo na pale wanaporusha moja kwa moja ni aibu.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura amesema ni kweli mitambo ya TBC imekuwa chakavu, lakini Serikali inaifanyia kazi na imeongeza bajeti ya shirika hilo kutoka Sh1 bilioni hadi Sh3 bilioni.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema hoja ya Bunge Live amekuwa akiijibu na anachoweza kusema ni kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA) imelikabidhi Bunge leseni na sasa litaweza kuamua lolote.
Pia alijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge kuhusu bajeti ya wizara yake. Juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii, akisema ni hatari na isipoangaliwa inaweza kuingiza nchi katika matatizo, hivyo lazima sheria zichukuliwe dhidi ya wanaokiuka matumizi yake.
Tupia Comments: