Wanakijiji wa kijiji cha Mngeta wakiangalia wadudu wanatumika kutathimini ubora wa maji ya mto
Nchini Tanzania, katika mkoa wa Morogoro, wilaya ya Kilombero, baadhi ya wanakijiji cha Mngeta wameanza kunufaika na mafunzo maalumu ya kutathimini ubora wa mito kwa kutumia viumbe hai, hasa wadudu wasio na uti wa mgongo.
Watafiti wamebaini kwamba, teknolojia ijulikayo kama miniSASS ndio njia nyepesi inayoweza kutumiwa na mtu mwenye kiwango chochote cha elimu na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na utafiti wa maabara, hivyo inaweza kusaidia jumuia za watumia maji kujua ni kwa kiwango gani vyanzo vya maji vimeathirika kutokana na shughuli za binadamu kama vile ukulima wa pembezoni mwa mto na shughuli nyengine kama vile kufua na kuchota mchanga.
Dk. Lulu Kaaya ambae ni mtaalamu wa utafiti akitoa maelekezo kwa wanakijiji wa kijiji cha Mngeta
Baada kukusanywa kwa wadudu na kufanyiwa tathmini, ndipo wanakijiji wanapobaini iwapo maji ya mto umeathirika kutokana na shughuli za binadamu au la, na hatimae kujua hatua gani za kuchukua.
Tanzania licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji, lakini baadhi ya vyanzo hivyo viko hatarini kutokana na shughuli za binadamu zinazoendelea pembezoni, kama vile kulima, kulisha mifugo na hata kuchota mchanga hivyo kusababisha mmomonyoko.
Ingawa kuna sheria inazuia matumizi mabaya ya vyanzo vya maji, lakini kila kukicha, kasi ya uharibifu inaarifiwa kuongezeka.

Tupia Comments: