SERIKALI imesema visiwa vyote vya bahari na maziwa yakiwemo Victoria, Tanganyika na Nyasa vitafikiwa na umeme. Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akizindua Bodi ya Umeme Vijijini.

“Visiwa vyote ndani ya miaka miwili au mitatu lazima vipate umeme, hatuwezi kupitisha ‘cable’ chini ya bahari au chini ya ziwa tutatumia umeme wa nguvu za jua,” alisema na kuongeza kuwa kazi hiyo itafanywa na kampuni binafsi ambazo zote ni za Watanzania.

Alisema pia Wakala wa Umeme Vijijini(REA) na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wamekuwa wakitofautiana kwenye takwimu za Watanzania ambao wana umeme vijijini. Profesa Muhongo alisema hadi kufikia Desemba 30,2016 wenye fursa ya kutumia umeme vijijini ilikuwa ni asilimia 49.5 na kwamba REA ilianza mwaka 2007 na mwaka 2008 ikaanza kazi na wakati huo wana vijiji wa Tanzania bara wenye fursa ya kutumia umeme ilikuwa ni asilimia mbili.

“Kutoka asilimia mbili hadi asilimia 49.5 ni hatua kubwa imepigwa... kwenye kikao cha kwanza mwenyekiti wa bodi uje na takwimu wajadili waweke malengo na mapendekezo yao wanataka ifike asilimia ngapi,” alisema na kuitaka bodi hiyo kuhakikisha inatoka asilinia 49.4 kwa kutoa makisio.

Waziri Muhongo alisema kwenye umeme kuna ile fursa ya kutumia umeme lakini kuna kipimo cha pili ni wale watu asilia waliofungiwa umeme. “Ni nani hasa kafungiwa umeme takwimu zinaonesha ni asilimia 16.9 ni lazima kutafuta uhalisia, mtatokaje kwenye 16.9 mtafika ngapi,” alisema.

Aidha alisema bado vijiji 7, 800 nchi nzima ambavyo havijafikiwa na umeme na kuongeza kuwa katika mradi wa REA awamu ya tatu utashughulika sana na na maeneo ya mbali na gridi

Tupia Comments: