Mauaji ya kutumia silaha za moto yameendelea kushamiri nchini,baada ya mfanyabiashara mmoja mjini Singida kufariki dunia baada ya kupigwa risasi ya bunduki aina ya bastola wakati akitaka kuondoka dukani kurejea nyumbani.
Mfanyabiashara huyo na mkazi wa Itungukia tarafa ya Mungumaji manispaa Singida ni Simon Charles (49).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa jeshai la polisi mkoa wa Singida,ACP Debora Magiligimba, alisema tukio hilo la kusikitisha limetokea Aprili, 20 mwaka huu saa 3.30 usiku.
Alisema siku ya tukio baada ya mfanyabiashara huyo kufunga duka lake la madawa ya binadamu lililopo standi ya zamani ya mabasi alianza kuelekea kwenye gari lake ili aweze kurejea nyumbani kwake.
“Wakati akikaribia gari lake ghafla muuaji huyo ambaye alijificha upande mwingine wa gari hilo alinyanyuka na kumpiga risasi titi la upande wa kulia na kutokea nyuma na kisha kudondoka pale pale. Wasamaria wema waliweza kumkimbiza hospitali ya mkoa lakini alifariki akipatiwa matibabu.Kifo chake kinatokana na kuvuja damu nyingi,” alisema Magiligimba.
Kamanda huyo alisema kwenye eneo la tukio kulipatikana ganda moja la risasi ya bastola. Hadi sasa chanzo cha mauaji hayo, bado hakijajulikana.
Katika hatua nyingine, Magiligimba alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na msako mkali kubaini watu waliojihusisha na tukio hilo ili waweze kukamatwa na sheria ziweze kuchukua mkondo wake.
“Jeshi la polisi linatoa wito kwa wananchi wote mkoani kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kusaidia kukamatwa kwa wauaji hao. Pia wafanyabiashara tunawakumbusha umuhimu wa kuajiri walinzi, watakaowalinda wao na mali zao,” alisisitiza.
Habari kutoka eneo la tukio, zinaeleza kwamba mfanyabiashara huyo ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu ameauwa na mtu mmoja ambaye alivalia suruali. Baada ya mauaji hayo, mtu huyo aliondoka kwa miguu na kutokomea kusiko julikana.
Mashuhuda wengine wanadai kuwa muuaji huyo hakuweza kukamatwa wala kufukuzwa, kwa madai kuwa mlio wa risasi ya bastola haukuwa mkubwa hivyo wakahisi kuwa ni tairi la pikipiki limepasuka na hivyo walipuuzia.
Tupia Comments: