Viongozi wa kundi la mataifa ya G20 wamekubaliana katika kulaani ghasia zilizofanywa na waandamanaji mjini hamburg lakini wameshindwa kuja pamoja katika mawazo yao kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi na biashara huru.       
Anaandika  mwandishi  wa  DW ,Bernd Roegart  kutoka  Hamburg kwamba  kansela  Angela  Merkel  ambaye  alikuwa  mwenyeji  wa  mkutano  huo  wa  kilele alijitokeza  katika  tukio  maalum mwishoni  mwa  mkutano  huo wa  G20, wakati  alipokutana na wawakilishi  wa  jeshi  la  polisi. Aliwashukuru kwa  kuweka  maisha  yao  katika  hatari kuhakikisha  usalama  kwa  viongozi  wa  nchi  na  serikali  pamoja  na  wajumbe  wao  wakati wakikutana  katika  mji  huo wa  kaskazini mwa  Ujerumani.
ansela wa Ujerumani  hakutafuna maneno  katika  shutuma  zake  kali dhidi ya  mapambano  ya  ghasia  ambayo  wanaharakati wanaopinga  utandawazi  walipambana  katika  siku  mbili  hapo  kabla. "Watu  ambao wanafanya hivyo hawana nia  ya  kukosoa  masuala  ya  siasa. Wale  wanaofanya  hivyo wanafanyakazi nje ya  jamii  ya  kidemokrasi." Merkel  pia  aliahidi  msaada  wa  haraka  kwa wahanga  wa  vitendo  vya  ghasia.
Marais katika  eneo  la  Schanzen mjini  Hamburg  na  vitongoji vya  Altona  hawakuwa  na hamasa  juu  ya  kazi  iliyofanywa  na  polisi. Vitongoji  hivyo vilikuwa  ni uwanja  wa  mapambano na  uporaji  na  uchomaji  moto  dhidi  ya  biashara  mbali  mbali , vitendo vilivyofanywa  na waandamaji waporaji , magari  kadhaa  yaliharibiwa  pia.
Mkaazi  mmoja  ambaye  alifadhaishwa aliweka  bango  kubwa  kutoka  katika  varanda  yake lililosomeka: "hiyo ilikuwa  ni  wazo  la kijinga Olaf." Olaf ni  Olaf Scholz, meya  wa  sasa  wa  mji  wa  Hamburg. Anahisika  na  kuuleta mkutano  wa  G20  mjini  Hamburg  na  aliwaahidi  wakaazi  kwamba  usalama  wao utahakikishwa wakati  alipozungumzia  wasi  wasi  wao  kabla  ya  mkutano  huo.
Usalama wahakikishwa
Hakuna  muandamanaji  aliyeweza  kufika  katika  eneo lililotengwa  kwa  ajili  ya  mkutano  huo , ambako  viongozi wa  mataifa  19 yenye  utajiri  mkubwa  wa  viwanda  pamoja  na  yale yanayoinukia  kiuchumi  pamoja  na  wawakilishi kutoka  Umoja  wa  Ulaya  walikutana  siku  ya Ijumaa  na  Jumamosi.
Jaribio  lolote  kufanya  hivyo  lilizuiwa  na  polisi  wapatao 20,000 na majeshi  ya  usalama  kutoka  Ujerumani  na  mataifa  jirani  ya  Umoja  wa  Ulaya.Ndani  ya  jengo la  maonesho  ya  biashara  ambako  mikutano  ilifanyika, taarifa  ya  mwisho  ya  pamoja iliwasilishwa  ambayo  ilibakia  kuwa  haieleweki  katika  maeneo  mbali mbali.
Mataifa  yote  20 yalikubaliana  kwa  pamoja  katika  imani  yao  kwamba utaratibu  wa  kudhibiti masoko  ya  fedha uendelee, pamoja  na  haja  ya  kupambana  na  hali  ya  kufadhili  ugaidi  na  ukwepaji  kodi. Masuala  haya  ni  msingi  wa  wasi wasi wa "serikali  za  dunia" ambao uliasisiwa  kama  jibu kwa  mzozo  wa  kifedha  wa  mwaka  2008.
Umoja , ambao  ni  utamaduni  wa  kundi  la  G20 , ulifikia  mwisho , hata  hivyo , katika  mada  ya kupambana  na  ongezeko  la  ujoto  duniani. Idadi  ya  waliokubali  ilikuwa  19 dhidi  ya  mmoja , kwa  kuwa  Marekani  hivi  karibuni  ilijitoa  kutoka  makubaliano  ya  Umoja  wa  mataifa  ya  mjini Paris kuhusiana  na  mabadiliko  ya  tabia  nchi.
Mjini  Hamburg , rais  wa  Marekani  Donald Trump  pia  alikataa  kutambua  upunguzaji  wa  utoaji gesi  hizo  zinazochafua  mazingira  uliomo  katika  makubaliano  ya  Paris.
Marekani yashikilia  msimamo wake
"Kila palipo  na  muafaka, ni  lazima pia kuna  mpinzani," kansela Angela  Merkel  alisema, na kuongeza  kwamba  anasikitishwa  na  ukweli  kwamba  Marekani imeachana  na muafaka  wa mazingira. "Nafarijika kwamba  kila  kiongozi  mwingine wa  taifa  na  serikali  anakiri  kwamba makubaliano  ya  Paris  hayawezi  kubadilishwa."
Merkel  amesisitiza  kwamba  makubaliano  yanapaswa  kutekelezwa  haraka  iwezekanavyo. Trump  alitoa  taarifa  ambayo  iliongezwa  katika  taarifa  ya  mwisho  ya  pamoja  na  kusema kwamba  Marekani  inataka  kusaidia  mataifa  mengine  kupata  njia  salama  za  kutumia  nishati za  makaa  ya  mawe , gesi  na  mafuta. Makubaliano  ya  Paris  yanataka  kusitishwa  kabisa kwa  matumizi  hayo.
Katika  mada  ya  biashara, wajumbe  wa  majadiliano  wa  G20 walitumia  siku  kadhaa wakipambana  na  upinzani  wa  Marekani  kabla  ya  hatimaye  kufikia  makubaliano. Hatimaye , mkutano  huo  wa  kilele  ulikubaliana  kuhusu  biashara  ya  haki  kwa  wote  na  kuonesha  nia  ya kuimarisha  taasisi ambazo  zinaweza  kutumika  wakati  ambapo  biashara  imekwazika.
Kama  ilivyokuwa  hapo  kabla , shirika  la  biashara  duniani  WTO litakuwa  kama  muamuzi. Uwezo wa  kuingia  katika  masoko  ulitajwa  pia. Suala  hilo  liliongezwa  kwa  kuiangalia  zaidi China , ambayo  inataka  kulinda  sana  makampuni  yake  dhidi  ya  ushindani  nyumbani  na wawekezaji  wa  kigeni. Donald Trump  alijitokeza  dhidi  ya  makubaliano  ya  biashara yanayohusu  makundi  ya  mataifa ,  kwasababu  alisema "hayatendi  haki" kwa  Marekani.
Anataka  makubaliano  ya  nchi  moja  moja, kama  vile  na  Uingereza, ambayo  inakaribia kujitoa  kutoka  Umoja  wa  ulaya  katika  muda  wa  miaka  miwili  ijayo.
Kuhami masoko
Hata  hivyo  kinyume  na  taarifa  nyingi  zilizotolewa  hadi  sasa, Trump  alisema  haamini  kuhusu kuhami  masoko. Kwa  hiyo  hii  inaonekana  kama  ushindi  mdogo  kwa  kundi  la  G20. "tunaweza  kufanikiwa  zaidi  wakati  tukichukua  hatua  kwa  pamoja  kuliko ukichukua  hatua peke  yako," amesema  kansela  Merkel.
Kansela  Merkel  pia  amefanikiwa  katika  kusukuma wazo  ambalo  analipenda  sana. G20 ikubaliane  kufanya  uwekezaji mpya  kwa  Afrika. matumaini  ni  kwamba  uwekezaji  wa  moja  kwa  maja  wa  mashirika  utatia  nguvu  uchumi  wa mataifa  ya  Afrika.
G20  inasema  pia  kwamba  inataka  kulisaidia  bara  la  Afrika kutumia  na  kuwezesha uwekezaji kwa  kuyapatia  mataifa  hayo  fedha  za  kuanzia. Ni  matumaini  kwamba  muktadha mpya  wa  kiuchumi  utawafanya  watu  wa Afrika  waache  kuhamia  katika  bara  la  Ulaya. Na  hii ni  kupitia  kile  kinachofahamika  kama "Mkataba  na  Afrika"  ambao  umekuwa  sehemu  ya mkakati  wa  Umoja  wa  Ulaya  wa  kupambana  na  uhamiaji.
Hata  hivyo , kuna  sehemu  kubwa  ya  kuweza  kuboreshwa. Kwa  hivi  sasa , Uwekezaji  wa Ujerumani  katika  bara  la  Afrika  unafikia  tu kiasi  cha  asilimia  moja  ya  jumla  ya  uwekezaji wa  kibiashara  za  kigeni  za  Ujerumani. Taasisi  za  serikali  za  China  zinaongoza  dunia katika uwekezaji  wa  moja  kwa  moja  katika  Afrika na  haipotezi muda  mwingi ikitia shaka  juu  ya masuala  ya   utawala  bora  katika  bara  hilo.
CHAZO - DW  SWAHILI

Tupia Comments: